NA LAYLAT KHALFAN
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), limeiomba serikali ya awamu ya nane kutekeleza ahadi iliyotolewa na serikali ya awamu ya saba ya kuongeza kima cha mshahara kwa watumishi wa umma.
Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Khamis Mwinyi Mohamed, alitoa ombi hilo ofisini kwake Kikwajuni alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari wakati akitoa tathmini ya mwaka 2020.
Alisema serikali ya awamu ya saba mnamo mwezi Aprili mwaka 2020, iliahidi kuongeza mishahara kwa wafanyakazi, hata hivyo ahadi hiyo ilishindwa kutekelezwa kutokana na ugonjwa wa corona.
Alisema ugonjwa wa corona ulisababisha mapato ya serikali kupungua kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi kufungwa, hata hivyo hivi sasa hali ya uchumi Zanzibar imeonekana kukua kwa kasi, hivyo ni vyema serikali kutekeleza ahadi hiyo.
Alifahamisha kuwa kutokana na kasi ya maendeleo kwa awamu ya nane, Shirikisho hilo linategemea serikali kuchukua hatua za haraka kutimiza ahadi hiyo kwa wafanyakazi wake.
“Tunaelewa kwamba mwaka 2020 kulikuwa na mtikisiko mkubwa kiuchumi duniani kutokana na mripuko wa corona, nchi zilizotegemea viwanda bidhaa zao zilikosa soko, zile zinazotegemea mafuta bei ilishuka na nchi zilizotegemea utalii wageni hawakuruhusiwa kutoka katika nchi zao lakini sasa hali tayari ishatengemaa kwa hiyo tunaiomba serikali itekeleze ahadi yake”, alisema.
Aidha, alieleza kuwa, kulingana na mfumo mpya wa mishahara kwa mashirika ya umma, mamlaka na taasisi zinazojitegemea, zinatarajia kupitiwa upya zoezi hilo ili kuondoa manung’uniko na kurejesha motisha na ari kwa wafanyakazi.
Akizungumzia kuhusu sekta binafsi, katibu huyo alisema kuna baadhi ya waajiri kutokutekeleza amri ya serikali juu ya malipo ya viwango ya mishahara na posho zilizowekwa pamoja na utaratibu wa kuajiri wageni.
Kuhusu mabadiliko ya sheria ya ZSSF na athari ya kupungua kwa kiinua mgongo kwa wanaostaafu, aliomba sheria hiyo ipitiwe upya ili iendane na hali ilivyokuwa kabla au kuwe na mpaka baina ya waliojiunga baada ya mabadiliko hayo.
Kuhusu madeni ya wafanyakazi wa serikali yakiwemo maposho ya likizo, saa za ziada, mazingira magumu, dhamana, tofauti za mishahara , nauli na nyongeza za mwaka, aliishauri kufanyiwe tathmini ya madeni ya wafanyakazi ili kuhakikisha yanalipwa kwa lengo la kukuza utendaji kazi katika taasisi.
Aidha, aliwashukuru viongozi wa awamu ya saba hususan Rais wa awamu hiyo, Dk. Ali Mohamed Shein sambamba na kumpongeza Rais wa awamu ya nane, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa ushindi mkubwa alioupata na hatua anazozichukua katika kuimarisha uchumi , huduma bora na haki za wananchi.
Sambamba na hilo aliwaomba viongozi, wafanyakazi na wananchi kushirikiana katika kuiunga mkono serikali iliyopo madarakani katika jitihada zake za kupiga vita rushwa, uzembe na ubadhirifu wa mali za umma.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Ali Mwalim Rashid, alisema kuchelewa kuanzishwa kwa vitengo muhimu kwa maslahi ya wafanyakazi ikiwemo, mfuko wa bima ya afya, mfuko wa fidia za wafanyakazi, chuo cha ubaharia, chuo cha uvuvi hivyo ni vyema kwa serikali kujitahidi kuendelea na utaratibu wa uanzishwaji wa vitu hivyo ili kuimarisha ajira nchini.
Mapema Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mahoteli na Majumbani (CHODAWU), Ally Salum Ally, aliiomba serikali kusimamia sheria ili kuhakikisha sekta binafsi zinatumia haki na wajibu kwa kila mfanyakazi.