NA ZAINAB ATUPAE

VIONGOZI wa Shirikisho la mpira wa miguu Zanzibar (ZFF) wametakiwa kuachana na tabia ya kuendesha soka kimazoea,badala yake watafute mbinu mbadala ambazo zitawasaidia kubadilisha soka hilo na kufikia malengo.

Ushauri huo umetolewa na kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21 Ramadhan Ahmada Iddi alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili.

Alisema uendeshaji wa soka uliopo ni wa kimazowea ambao unarejesha nyuma soka hasa kwa viongozi wa timu.

 “Uendeshaji wa kimazowea huu unarejesha nyuma soka letu na kama hatutokubali kubadilika tutaendelea kuwa nyuma kila siku,”alisema.

Alisema umekuwa na udanganyifu mkubwa kwenye timu hasa wakati timu zinapocheza mechi zao, ambapo baadhi ya  timu hupendelewa na kupata ushindi hata kama uwezo wao wa kushinda mdogo.

Akizungumzia juu ya utofauti uliopo kati ya soka la zamani na sasa,alisema kuna tofauti kubwa kwani zamani wachezaji walikuwa wakicheza kwa uzalendo zaidi,lakini wachezaji wa sasa wanacheza kimasilahi.

“Zamani wachezaji walikuwa wakicheza kwa uzalendo na kuweka heshima ya mitaa yao,na ndio maana timu za vikosi zilikuwa tatu na timu za mitaani ziko nyingi na zinafanya vizuri,lakini sasa ligi kuu inatawaliwa na timu za vikosi,”alisema.