NA NAFISA MADAI

KAIMU Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA), Zaidi Ramadhan Taufiq amesema mamlaka hiyo inakabaliwa na changamoto ya kutoridhiwa mikataba ya kimataifa kwa nchi wanachama wa shirika la kimataifa la masuala ya bahari (IMO).

Kaimu huyo alisema hayo jana alipokua akisoma ripoti ya utelelezaji wa bajeti kwa kipindi cha miezi sita Julai hadi Disemba kwa kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi katika ofisi za Mamlaka zilizopo Malindi mjini Zanzibar.

Aidha alisema kutoridhiwa kwa mikataba hiyo nchi ya Tanzania, kunasababisha   bendera ya Tanzania kuonekana haiko makini katika kusimamia usajili wa meli zake.

Hata hivyo, alisema hali hiyo imetokana na baadhi ya meli zilizowahi kusajiliwa na Tanzania kubeba dawa za kulevya na silaha kwa njia ya haramu, ambapo serikali ya Jamhuri wa Muungano ilipotoa agizo kwa mamlaka kusitisha usajili wa meli za kimataifa.

Alisema kusitishwa kwa zoezi la usajili wa meli za kimataifa na Mamlaka hiyo kumesababisha upungufu mkubwa wa mapato.

Kaimu huyo alisema licha ya kuwa mamlaka ya usafiri baharini ina uwezo kisheria wa kukusanya ada ya mafuta yanayoingizwa nchini, lakini kwa sasa kanuni hiyo imefutwa tokea mwaka uliopita jambo ambalo pia alisema mamlaka imepoteza chanzo chengine cha mapato.

Sambamba na hayo, aliiomba kamati hiyo kuyafuatilia kwa ukaribu zaidi masuala hayo ili mamlaka iweze kurejeshewa huduma hizo kwa maslahi ya nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Panya Ali Abdallah alieleza kusikitishwa na hali hiyo ambapo alisema imefika wakati kukaa tena kwa serikali zote mbili kujadiliana kwa kina ili kuhakikisha suala la usajili wa meli za kimataifa linamalizika.

Hata hivyo, alisema tatizo la kutosajili meli za nje si la kulifumbia macho tena kwa vile serikali imekua ikikosa mapato ambayo yangeweza kuchangia maendeleo ya Zanzibar.

Aidha mwenyekiti huyo alisisitiza suala la usajili wa vyombo vidogo wahakikishe wanavisajili na kuvifanyia ukaguzi wa mara kwa mara ili kunusuru maisha ya abiria na mizigo wanayopakia katika vyombo hivyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mustafa Aboud Jumbe alisema suala la usajili wa meli za kigeni serikali iliagiza uangaliwe upya kutokana na baadhi ya meli kukiuka makubaliano ya usajili.