Wananchi wana matumaini kibao kupatika rasilimali hiyo

Rais mstaafu Dk Shein ataka wananchi kuwa na subira

NA MWAJUMA JUMA

ILI kuona uchumi wa Zanzibar unakuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba. ilianza harakati za utafutaji wa mafuta na gesi asilia Unguja na Pemba kuanzia mwaka 2017, mara baada ya kuwepo kwa tetesi za muda mrefu za kuwepo kwa rasilimali hiyo.

Uamuzi huo ulipelekea kutungwa kwa sera ya mafuta na gesi asilia ya mwaka 2016 na baadae sheria ya mafuta na gesi asilia nambari 6 ya mwaka 2016, ambayo inaweka misingi ya uendeshaji wa shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na usimamiaji wa biashara hiyo.

Aidha, kampuni ya maendeleo ya mafuta na gesi asilia ZPDC nayo imeanzishwa chini ya kifungu cha 32 cha sheria hiyo na kusajiliwa chini ya sheria ya makampuni nambari 15 ya mwaka 2013.

Kampuni hiyo ni mkono wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusimamia na kushiriki kwenye utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na katika biashara inayoambatana na rasilimali hiyo.

Kampuni hiyo pia inajukumu la kulinda maslahi ya taifa katika biashara hiyo, ambapo katika utekezaji wa kazi zake imetayarisha mpango mkakati wa miaka mitano ambao unaelekeza uendeshaji wa kampuni na mipango yake ya maendeleo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2019 hadi 2023.

Miongoni mwa mikakati iliyomo katika mpango mkakati huo ni kujenga uelewa wa jamii juu ya shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia hadi uchimbaji kama yatapatikana.

Aidha, katika mazingira ya minong’ono mingi ambayo huambatana na kupeana matumaini makubwa au kukatishana tamaa kwa misingi ya uvumi, ni muhimu kuwepo kwa utaratibu rasmi wa kuelimisha umma kwa uendelevu.

Kwa kuwa sekta ya mafuta na gesi asilia ni mpya hivyo ushirikishwaji wa wananchi katika kujiandaa kupokea mabadiliko ya kiuchumi ni muhimu kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.

Hivyo, katika kulijua hilo, ZPDC hivi karibuni ilitoa mafunzo kwa wajumbe wapya wa Baraza la Wawakilishi yenye lengo la kuwatayarisha na kuelewa uchumi wa mafuta na gesi na maslahi ya taifa.

Katika mafunzo hayo wajumbe hao walipata mafunzo yaliyotokana na mada mbali mbali huku mada kuu ikiwa ni ya uzalendo kwa maslahi ya taifa lao.

Mwanasheria wa Kampuni, Walid Mohammed Adam, anasema, wameanza na wajumbe hao wawakilishi kwa sababu wameona wana kundi kubwa la watu ambao linawazunguka na wanataka wapate taarifa sahihi.

“Tulifanya mafunzo ya siku tatu kwa waheshimiwa wawakilishi yaliyoanza Novemba 22-24 mwaka huu, ambayo yaliendeshwa na wataalamu kutoka Chuo cha Demokrasia Dar es Salaam kilichopo Kurasini

Alisema kuwa madhumuni ya mafunzo hayo ni kuwatayarisha wawakilishi kuelewa sekta ya uchumi wa mafuta na gesi na maslahi ya taifa kwa ujumla wake.

“Tunajua baada ya taarifa ile ya rais kuhusiana na taarifa ya zoezi la utafiti juu ya utafutaji wa mafuta na gesi watu wamejawa na matarajio makubwa, ni vizuri, lakini, tunataka wapate taarifa zilizosahihi na kwa watu sahihi”, alisema.

KWANINI TUKAZUNGUMZIA MASLAHI YA TAIFA NA UZALENDO?

Anasema, taasisi hiyo kwa makusudi iliamua kutoa mafunzo hayo hasa kwa kuwa kampuni kadhaa za kimataifa ndizo zenye uwezo wa kifedha, kiutaalamu ndizo zitakazotafuta rasilimali hiyo.

“Kwa kuwa Zanzibar ndio kwanza wanaanza, lakini, uzoefu uliojitokeza katika nchi nyengine duniani wameona kuna nchi mbali mbali zenye matatizo ya rushwa, umasikini hali ya kuwa rasilimali zinapatikana na kuzalishwa kwa wingi”, alisema.

Hivyo, anasema serikali haitaki kuona rasilimali na maliasili hayo yanaingia katika sintofahamu na kwamba rasilimali hiyo iwanufaishe wazanzibari wote na Zanzibar kwa ujumla wake.

Kwa upande wake, Ofisa Dhamana Idara ya Fedha ya Kampuni hiyo, Abdulhalil Hassan Ramadhan, anasema, lengo kuu la uchumi na mafuta na gesi ni kuwaelezea wawakilishi jinsi gani sekta tofauti tofauti zinaweza kusimamia uendeshaji wa mafuta na gesi nchini.

Anasema kuwa katika suala hilo watu wanapaswa kuelewa kwamba sekta ya mafuta na Gesi Asilia haisimamiwi tu na kampuni moja na ieleweke kuwa ni mtambuka.

“Isiwe kampuni tu ya ZPDC na Mamlaka ya Udhibiti na Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar ZPRA ndio wenye jukumu la kusimamia isipokuwa kuna sekta tofauti kama wao ZPDC, ZPRA, CAG, AG, Baraza la wawakilishi na sekta kama za uvuvi.

“Zote hizo kwa ujumla ndio zitawapelekea manufaa nchi, kwa sababu mafuta yanatafutwa baharini ambapo kuna taasisis tofauti ambazo ndizo zilizolengwa kwenye uchumi na mafuta na gesi”, anasema.

KUHUSU SHERIA

Walid, anasema, sheria namba sita ya mwaka 2016 ni sheria ambayo inasimamia shughuli nzima ya uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi mpaka unachimba na kuyapata na nini kifanyike mara tu unapomaliza uzalishaji.

Anasema sheria hiyo imekuja kuunda vyombo ambavyo vinasimamia mafuta na gesi ambavyo ni ZPRA ambayo jukumu lake kubwa ni kusimamia na udhibiti wa mafuta.

“Mafuta na gesi ni sekta mtambuka ina kila eneo limeingia sasa hapo mamlaka inajukumu la kusimamia shughuli nzima ikiwemo kuishauri Serikali”, alisema.

Aidha, anasema, sheria hiyo pia imeanzisha kampuni ya maendeleo ya mafuta katika kifungu cha 32 ambayo imeipa majukumu makubwa matatu ikiwemo kusimamia maslahi taifa katika mafuta na gesi asilia, kushiriki kwenye zoezi la utafutaji mafuta na gesi asilia kwa niaba ya Serikali na kuwa chombo cha kibiashara kwa niaba ya Serikali.

Hivyo, anasema, sheria hiyo pia imezungumzia ushiriki wa Wzanzibari katika biashara hiyo ya mafuta na gesi, lengo likiwa ni kwamba mafuta na gesi yanamnufaisha kila mwananchi.

 “Biashara hii ni hatari hakuna mtu ambae atakubali kirahisi kuingiliwa eneo lake, sasa hutumia njia hizi ili kuweza kufanikisha mipango yao hiyo”, alisema.

Hivyo, alitahadharisha kuwa mataifa mengi yenye rasilimali hiyo au yanayotaka tenda ya kutafuta na kuchimba yana ushindani wa kibiashara jambo ambalo hupelekea kutumia fedha nyingi kuwashawishi wanasiasa kwenye sheria ili kupenyenza vifungu ambavyo vilegezwe ili na wao waweze kunufaika.

“Kwa muktaza huu tumekwenda katika wakati muafaka kwani tumeweza kuwapa mafunzo ya kuona huko wanakokwenda kuna uchumi wa mafuta na gesi asilia hivyo hayo yatajitokeza na hivyo kila mmoja aweke maslahi ya taifa ili Zanzibar inufaike leo na vizazi vijavyo”, alisema Walid.

Akitoa tahmini alisema kwa sasa Zanzibar kuna miamba inayohifadhi mafuta na gesi, ila hakuna utaalamu unaoweza kuthibitisha kuwepo mafuta ama gesi bali mpaka upembuzi yakinifu sambamba na utafutaji wake uchukuwe miaka kadhaa jambo ambalo kwa sasa limeanza kwa baadhi ya mambo.

MAFANIKIO YA KAMPUNI

Katika kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwake imepata mafanikio mbali mbali ikiwemo kusaini mkataba wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na mafuta na gesi asilia na kampuni ya Ras Alkhaimah kwa kitalu cha Pemba – Zanzibar.

Kuandaa mpango makakati wa miaka mitano 2019-2023, ambao unaelezea mipango ya kampuni katika ushiriki wake kwenye utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, kuandaa kanuni na miongozo ya utendaji wa kampuni, iongozo ya uajiri, kanuni za usimamizi wa fedha na kanuni za watendaji.

Kushiriki katika makongamano na ziara za kimafunzo yanayohusiana na masuala ya mafuta na gesi asilia jijini Dar es Salaam-Tanzania, Uganda, Mombasa Kenya na Kuala Terengnanu –Malaysia, kushiriki mafunzo ya vitendo Tanzania Bara katika uchimbaji wa visima vya utafiti kupitia Shirika la maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC).

Kufanya mikutano ya kutoa uelewa kwa baadhi ya taasisi ambazo ni wadau wa sekta ya mafuta na gesi asilia ambapo hadi sasa kampuni imeshakutana na taasisi zinazohusika na elimu, ulinzi wa baharini, utalii, Mamlaka ya Kudhibiti Huduma za Maji na nishati na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).

Kampuni imeanza uajiri wa wataalamu sita wa kada tofauti za mafuta na gesi asilia, wataalamu hao ni wa kada ya uhandisi wa mafuta, jiologia na jiofizikia.

CHANGAMOTO

Mbali na kuwa na mipango hiyo lakini kampuni hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na uhaba wa uzoefu katika sekta ya mafuta na gesi asilia.

“Kwa kuwa sekta hiyo bado ni mpya na ni nchi ina wataalamu wachache wenye uzoefu wa kutosha katika masuala ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ni changamoto kubwa kwa sasa”, alisema.

Hata hivyo, anasema ili azma hiyo ifanikiwe ni lazima wananchi kuonesha ushirikiano mkubwa na kampuni na wafanyakazi wa sekta hiyo.

WANAVYOZUNGUMZA WANANCHI KUHUSIANA NA RASILIMALI HIYO

Ali Mtumweni Khamis ambao ni miongoni mwa wanakijiji waliopisha mradi wa mafuta na gesi asilia katika kijiji cha Bumwini Dundua, alisema kwa kuwa serikali lengo lake ni kuleta maendeleo basi kama wakaazi wa eneo hilo hawanabudi kukbaliana nayo.

“Tumejemngewa na kusogezewa huduma zote rafiki tumelikubali kwa roho safi tunaahidi kushirikiana na serikali yetu ili kutuletea maendeleo ya dhati”, alisema.

Nae Azizi Shaibu Rajab, akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Dundua wameishukuru serikali kwa hatua walioichukua ya kuwajengea nyumba bora na kuahidi kuzitunza nyumba hizo ili ziweze kudumu.

Kiujumla wake wananchi wa Unguja na Pemba hasa sehemu zinazotazamiwa kupita rasilimali hiyo, wamefurahia hatua ya serikali iliyofikia na kwamba wako bega kwa began a serikali katika kila hatua ili kuona kwamba rasilimali hiyo ya wananchi na taifa kwa ujumla inapatikana hapa Zanzibar.

Jumla ya nyumba 31 zimejengwa na serikali kwa ajili ya kulipa fidia wakaazi wa kijiji cha Dundua ili kupisha uekezaji wa gesi na mafuta

ALIYAYASEMA RAIS MSTAAFU DK. ALI MOHAMED SHEIN KUHUSU MCHAKATO WA MAFUTA NA GESI ASILIA

Rais huyo mstaafu alisema Shughuli ya uchukuaji wa taarifa kwa njia ya mtetemo ilianza mwezi Oktoba 2017 na kumalizika mwezi Machi, 2020. Shughuli hio, ilifanywa na Kampuni ya BGP ya Jamhuri ya Watu wa China. Shughuli iliyofanywa ilijumuisha uchukuaji wa taarifa kutoka baharini, nchi kavu na katika kina kifupi cha bahari.

Kwa upande wa bahari, zoezi lilifanywa kwenye eneo lenye urefu wa kilomita 2,815.6, likijumuisha jumla ya mistari 66. Kwa upande wa nchi kavu, uchukuaji kwa njia ya mtetemo, ulifanywa katika jumla ya mistari 25 yenye urefu wa kilomita 717.1. Kadhalika, katika maeneo ya kina kifupi cha maji, zoezi lilifanywa kwenye mistari 10 yenye urefu wa kilomita 244.

“Baada ya kukamilika shughuli hizo za ukusanyaji wa taarifa, hatua iliyofuata lilikuwa ni kwenda kuzifanyia uchambuzi taarifa hizo, kazi ambayo ilikwenda kufanywa na kampuni ya BGP katika kituo hio kilichoko Kuala Lumpa nchini Malaysia.

“Usafirishaji wa taarifa za baharini umechukua miezi 11 (Januari, 2018 hadi Disemba 2018). Usafirishaji wa taarifa za nchi kavu na kina kifupi cha maji kwa maeneo ya Unguja na Pemba ulichukua muda wa miezi minane (8) kuanzia mwezi Oktoba, 2018 hadi mwezi wa Julai, 2019.

Matokeo ya usafirishaji wa taarifa zilizokusanywa yameonesha kuwepo kwa sura mbili tafauti. Kwa upande wa Unguja, taarifa za mistari zimekua na ubora unaoridhisha na kuonesha maeneo ya miamba yenye maumbile yanayoweza kuhifadhi mafuta na gesi asilia. Kwa upande wa Pemba, imeonesha taarifa zenye kiwango kidogo cha ubora kutokana na maumbile ya kijiografia ya kisiwa hicho (Gegraphical Landscape).

Kutokana na matokeo hayo, Kampuni ya RAK Gas imeonesha nia ya kutaka kuifanyia usafishaji wa mara ya pili, mistari yote yenye kiwango kidogo cha ubora, ili kuongeza ubora wa taarifa hizo. Kufuatia uamuzi huo, Kampuni ya RAK Gas ilichukua hatua ya kuendelea na kazi ya kutafuta taarifa za mitetemo za mafuta na gesi asilia kwa kitalu cha Pemba – Zanzibar, kazi ambayo ilianza mwezi Agosti, 2019 na kukamilika mwezi Machi, 2020.

Matokeo ya kazi waliyoifanya, yamepelekea Kampuni ya RAK Gas kuendelea na kazi ya kufanya uchunguzi kwa njia ya mtetemo katika kina kifupi cha maji, eneo ambalo linaonesha kuwa na viashiria vya kuwepo kwa gesi asilia.

Matokeo ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya Anga (Full Tensor Gradiometric Survey) na Mtetemo (2D Seismic Survey) yameonesha uwezekano mkubwa wa kuwepo miamba yenye uwezo wa kuhifadhi Mafuta na Gesi Asilia katika kitalu cha Pemba – Zanzibar.

“Hii ni kwa sababu, matokeo ya taarifa zote yameonesha kuwepo kwa viashiria vyote vya mfumo wa uhifadhi wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia (Petroleum System Elements (PSE). Kwa hakika hio ni taarifa njema na tumshukuru Mwenyezi Mungu.

BAADHI ya Mitambo iliyomo ndani ya Ndege Maalum ya Kampuni ya Bell Geospace Interprises Limited iliyofanya utafiti wa Rasilmali ya Mafuta Zanzibar.

UFUATILIAJI WA NJIA YA ANGA NA MTETEMO

Kwa upande wa utafutaji kwa njia ya anga, imeonekana kuwepo kwa maeneo matatu (3) yenye uwezekano wa kuwepo kwa miamba inayoweza kuzihifadhi rasilimali ya mafuta na gesi asilia. Maeneo hayo ni kisiwa cha Makoongwe kilichopo kusini mwa kisiwa cha Pemba, Kisiwa cha Tumbatu kilichopo Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Unguja na katika upande wa bahari ya Mashariki mwa kisiwa cha Unguja.

“Kwa upande wa utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya mitetemo, matokeo yameonesha kwamba yapo maeneo matano (5) yenye uwezekano wa kuwepo na rasilimali ya gesi asilia katika Kitalu cha Pemba – Zanzibar.

Sehemu zenyewe ni eneo la bahari liliopo baina ya Kaskazini Mashariki mwa kisiwa cha Unguja na Kusini mwa kisiwa cha Pemba, eneo la Kaskazini, Kusini na Mashariki mwa kisiwa cha Unguja, eneo la bahari ya Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Unguja, eneo la bahari ya Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Pemba na eneo la Kusini mwa Kisiwa cha Pemba.

Kwa jumla, maeneo hayo yameonesha kuwepo kwa maumbile ya miamba (Structures) yenye uwezo wa kuhifadhi rasilimali ya gesi asilia yenye ujazo wa futi trilioni 3.8.

Kwa mujibu wa tafsiri hio, uwezekano wa kufanikiwa kuigundua rasilimali ya gesi asilia wakati wa kisima ni asilimia thelathini (30%) kiwango ambacho ni kikubwa kwa upande wa utafutaji kwa njia ya mtetemo (2D Seismic). Aidha, kuna uwezekano wa kupanda kutoka asilimia thalathini (30%) hadi asilimia arubaini na tano (45%) baada ya kukamilika utafutaji wa kina kwa njia ya mtetemo kwa kutumia teknolojia ya 3D.

“Baada ya kupata matokeo hayo ya utafutaji, kwa njia ya anga na mitetemo yenye kutia matumaini, kazi zinazoendelea hivi sasa ni kama zifuatazo:-

i. Kuzifanyia usafirishaji wa mara ya pili taarifa zilizoonekana kutokuwa na ubora wa kuridhisha katika zoezi la mtetemo lililokamilika.

ii. Kuendelea na utafutaji rasilimali hizi katika kina kifupi kwa njia ya mtetemo kwenye maeneo maalum yaliyogundulika kuwa na viashiria vya kuwepo kwa mafuta na gesi asilia.

iii. Kutambua eneo la kuchimba kisima cha utafutaji (Identification of well location)

iv. Kuanza kazi ya kuchimba kisima cha kwanza cha utafutaji (Exploration Well Drilling).

Hizo ndizo shughuli kubwa zinazotaka kutekelezwa katika jitihada za Serikali yenu za kushughulikia rasililmali za mafuta na gesi asilia.

Kwa hakika, dhamira njema ya Serikali yenu ya kulishughulikia suala la utafutaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia inazidi kuonekana, kwani matokeo ya kazi ya utafutaji na uchambuzi wa taarifa za anga na mtetemo yanazidi kuleta matumaini ya kuwepo kwa uwezekano wa kugundulika kwa rasilimali hizo hapa Zanzibar.

“Viashiria vilivyobainika katika tafiti zilizokwishafanywa, vimeonesha matumaini ya kuwa na rasilimali hizo. Hata hivyo, katika utafiti uliofanywa, Kampuni ya RAK Gas imevutiwa kuvutiwa zaidi kuendeleza shughuli zake kwenye rasilimali ya gesi asilia katika maeneo ya baharini.

Pamoja na hayo, juhudi kubwa zinazohitajika katika kusimamia, kudhibiti na kuendeleza sekta ya mafuta ya gesi asilia kutokana na kuwa kazi hii huchukua muda usiopungua miaka sita (6) hadi minane tangu pale utafiti ulipoanza kufanywa; kabla ya kunufaika na rasilimali hizo.

“Kwa mara nyingine, napenda nikuelezeni kuwa shughuli hii si ya kukamilika na kuanza kunufaika kwa leo na kesho. Shughuli hio, bado itachukua muda usiopungua miaka sita mpaka minane tangu kuanza utafiti, kabla ya kuanza kunufaika na rasilimali hizi.

“Hata hivyo, Rais huyo mstaafu aliwataka wananchi kutovunjika moyo. Kwa hivyo, kuendelee kuwa na subira kwani wazee walisema, “Subira huvuta kheri.” Nina mategemeo makubwa kwamba huko mbele tutaweza kufaidika na rasilimali hizi kwa vile, tumefikia hatua nzuri ambapo tayari tumeandaa sera, Sheria na tumeanzisha taasisi za kushughulikia rasilimali hizi kufikia hatua nzuri za utafiti pamoja na kufanya maandalizi ya ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi huko Mangapwani katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

“Ninapomalizia kipindi changu cha Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, nimeridhika sana na hatua tulizozifikia katika kuishughulikia rasilimali ya mafuta na gesi asilia kama ilivyobainishwa kwenye Ilani ya uchaguzi Mkuu wa CCM ya mwaka 2015 na kwenye Ibara ya 96(b) ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020.