NA MADINA ISSA

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imezuwia kuendelea kwa ujenzi wa kituo cha kuuzia mafuta katika eneo ya Fuoni Kibonde Mzungu nyumba ya duara hadi itakapojiridhisha.

Akizungumza na vyombo vya habari katika eneo la kituo hicho, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Mbarak Hassan Haji, alisema miongoni mwa sababu zilizopelekea kufanya hivyo ni mazingira ya eneo hilo kuwa karibu na makaazi ya watu.

Alisema awali eneo hilo lilikuwa na ukubwa wa kutosheleza lakini kwa sasa limepungua kiwango cha ukubwa kutokana na harakati mbali mbali na kupelekea kutokidhi kujengwa kwa kituo hicho kwa mujibu wa sheria.

Mbarak aliitaja sababu nyengine kuwa ni uwepo wa karibu na kituo hicho kuendeshwa shughuli za soko linalotumiwa na watu wengi hivyo kutasababisha kuongezeka kwa msongamano hali inayoweza pia kuathiri usalama wa wananchi.

 “Awali tulipopokea barua ya kuomba kibali cha ujenzi wa kituo hiki tulikubali kijengwe kwani eneo lilikuwa linakidhi vigezo ila kwa sasa haitowezekana kutokana na kukusanya wananchi wengi,” alisema.

Nao baadhi ya wakaazi wa eneo hilo, walipongeza uamuzi huo kwani umeonesha kujali usalama wao na kuiomba serikali kutotoa kibali kwa kuendelea na ujenzi huo kabla ya kujua usalama wa wananchi wake.