NA KHAMISUU ABDALLAH

MWANAMME mwenye umri wa miaka 37, aliyedaiwa kujaribu kujiua mwenyewe kwa kutumia shati lake, amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo alitambulika kwa jina la Massoud Abdalla Mgereka mkaazi wa Kama wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Akiwa mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mdhamini wa mahakama hiyo Mohammed Subeit, mshitakiwa huyo alisomewa shitaka hilo na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Simni Mohammed.

Hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo ilidai kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kujaribu kujiua, kinyume na kifungu cha 198 na 26 (1) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa Masoud, alidaiwa kuwa Disemba 7 mwaka 2020 saa 8:10 mchana huko Polisi Ng’ambo wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alijaribu kujiua yeye mwenyewe kwa kutumia shati lake, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Hakimu Subeit, alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Machi 23 mwaka huu na kuutaka upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Pia mahakama, ilimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 500,000 za maandishi yeye mwenyewe na kuwasilisha mdhamini mmoja, atakaemdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi pamoja na kuwasilisha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na barua ya Sheha inayoonesha nambari ya nyumba.

Mshitakiwa huyo alikamilisha masharti hayo na yupo nje kwa dhamana hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.