NA RAMADHAN MAKAME

WAZEE wetu walituachilia urithi wa msemo mashuhuri wa kiswahili unaoeleza, ‘fanya wema wende zako…’, kwa hakika maisha ya uongozi wa Dk. John Pombe Magufuli yaliakisi msemo huo.

Katika maisha yake ya miaka mitano na miezi michache akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Magufuli amewatendea mema mengi watanzania, wakati wananchi wakirataji kuendelea kuwa naye ghafla kifo kimemnyakua.

Niseme tu siwezi kuelezea kila kitu katika uchambuzi huu katika kutathamini miaka mitano ya miezi michache ya maisha ya Dk. John Magufuli, akiwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, alikuwa kiongozi wa aina yake na kwa hakika wananchi wengi wa Tanzania walikuwa na matumaini makubwa kwamba uwepo wake katika uongozi unaweza kufanya makubwa kiasi cha kuipaisha Tanzania.

Jambo kubwa zaidi ambalo binafsi nitamkumbuka kiongozi huyo ni jitihada zake zilizofanikisha kuitoka katika orodha ya nchi masikini na kuipeleka hadi kuwa miongoni mwa mataifa yenye uchumi wa kati.

Tangu Tanzania ipate uhuru na Zanzibar kufanikisha mapinduzi, nchini imekuwa ikiitwa nchi masikini na kuna wakati ilikuwa miongoni mwa nchi masikini zaidi, isiyojiweza kwa lolote na hata kushindwa kulipa mzigo mkubwa wa madeni kwa mashirika ya kimataifa na mataifa wakopeshaji.

Kwa ujasiri mkubwa Magufuli aliwaeleza Watanzania kwamba Tanzania sio nchi masikini, na haya aliyasema kutokana na rasilimali nyingi ambayo nchi hii imejaaliwa haiwezi kuwa miongoni mwa nchini masikini.

Haikuwa rahisi wananchi wa Tanzania ambao kwa takriban miongo sita kila viongozi waliomtanguliwa kila wanapopanda majukwani wanaeleza kuwa hii nchi masikini, iweje Magufuli aseme hii si nchi masikini?

Katika kipindi cha miaka yake mitano tu kwenye uongozi watanzania waliamini yale aliyokuwa akiyasema na kwamba Tanzania ikatoka kwenye mstari wa nchi masikini zaidi duniani na kuingia kwenye kipato cha uchumi wa kati.

Hii ni miongoni mwa zawadi kubwa aliyowaachilia watanzania, kwani hivi sasa  uchumi upo vizuri, nchi inakopesheka, nchi inamudu kugharamia miradi kwa fedha za ndani bila ya mkopo ya nje, zaidi ya yote nchi inajitegemea kibajeti.

Hayo yote ameyawezaje? Ameyamudu haya kutokana na kusimamia vyema matumizi ya rasilimali za nchi, amesimamia matumizi ya fedha, amehakikisha anapiga vita rushwa na kadhalika.

Changamoto hizo tatu kubwa pamoja na nyengine ndizo zilizokuwa zikiifanya nchi hii ielekee siko na wananchi wengi kuamini kuwa watanzania kama vile wameumbwa kuwa masikini hadi kiyama.

Dk. John Magufuli kama binaadam wa kawaida anaweza asiwe sahihi kwa asilimia 100, na hilo linatokana na kwamba Mwenyezi Mungu ametuumba kila mtu kumpa mawazo yake, lakini wakati akiwa ameshafariki watanzania wengi wanamkumbuka kwa wema ama ubaya?

Jawabu ni moja tu, Dk. Magufuli anakumbukwa kwa wema wake aliowafanyia watanzania, anakumbukwa kwa jitihada zake za kuwaletea maendeleo watanzania, anakumbukwa kwa ujenzi wa miradi mikubwa aliyoijega kwa ajili ya watanzania.

Kitu kimoja lazima tukumbuke watu wema huwa hawapendezi katika kaumu zao ndio maana zipo baadhi ya nchi hapa Afrika wananchi wa mataifa hayo walitamani Dk. Magufuli awe kiongozi wao tena wanatuonea ‘chorozi’.

Watanzania kwa sababu tulikuwa naye hatutanabahi wala kuelewa kwamba huko nje Magufuli ni lulu, kweli huwezi kujua thamani ya kitu hadi kikutoke.

Kurasa za kitabu cha Magufuli zimefungwa, ni nafasi ya kuiangalia mbele kwa matumaini na sio kwa woga wala hofu, tuzitumie falsafa za magufuli na viongozi wengine kama hadidu rejea za kuipeleka Tanzania tunaikoitaka.

Buriyani Dk. John Pombe Magufuli, kwa hakika umeakisi msemo wa kiswahili unaosema ‘fanya wema wende zako’.