NA KHAMIS AMANI

MAHAKAMA ya mkoa Vuga, imeutaka upande wa mashitaka unaosimamia kesi ya unyang’anyi wa kutumika silaha, kuifanyia marekebisho hati ya mashitaka ili iendane na shitaka lililoainishwa.

Hakimu Makame Mshamba Simgeni, ametoa agizo hilo baada ya kubainika kasoro za kisheria zilizojitokeza katika hati hiyo.

Alifahamisha, maelezo ya kosa hayaendani na shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha lililowasilishwa mahakamani, kwa sababu haikuainisha ni aina gani ya silaha iliyotumika katika utendaji wa tukio hilo.

Hivyo kutokana na kasoro hizo, Hakimu Makame ameutaka upande huo wa mashitaka kuifanyia marekebisho hati hiyo katika kikao kitakachofuata, ili hati hiyo iyendane na shitaka hilo la unyang’anyi wa kutumika silaha.

Mapema, wakati mshitakiwa wa kesi hiyo alipokana shitaka hilo mara baada ya kusomewa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, upande wa mashitaka umebaini kasoro za kisheria na kuiambia mahakama itaifanyia marekebisho hati hiyo ya mashitaka katika kikao kijacho.

Mshitakiwa wa kesi hiyo ni Omar Khamis Mussa (20) mkaazi wa Magogoni wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, ambaye alishitakiwa mahakamani hapo kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Tukio hilo lilidaiwa kutendeka Februari 30 mwaka jana majira ya saa 10:00 za usiku, huko Welezo wilaya ya Magharibi ‘A’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Siku hiyo mshitakiwa huyo akiwa na wenzake, walidaiwa kushirikiana kwa pamoja na kwa kutumia nguvu, walimnyang’anya Massoud Mashaka Mustafa pikipiki aina ya TVS yenye nambari za usajili Z 986 KR, ikiwa na makisio ya thamani ya shilingi 2,900,000 mali ya Mwanakhamis Ali Salami.

Kesi hiyo inatarajiwa kufikishwa tena mahakamani hapo Machi 30 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi, kutokana na upelelezi wake tayari umeshakamilika.

Mshitakiwa huyo yupo rumande, kutokana na shitaka hilo linalomkabili ni miongoni mwa mashitaka yasiyokuwa na dhamana, kwa mujibu wa kifungu cha 151 (1) cha sheria namba 7/2018 sheria za Zanzibar.