KHARTOUM, SUDAN

WAZIRI wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan amesema kuwa, nchi yake haina nia kuzusha vurugu na machafuko nchini Ethiopia au kuingia katika vita na nchi hiyo jirani.

Mariam al-Sadiq al-Mahdi alisema hayo mjini Khartoum katika mazungumzo yake na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo na kueleza kwamba, nchi yake iko tayari kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi hitilafu za mpaka baina yake na Ethiopia.

Kwa upande wake Olusegun Obasanjo alisema kuwa, hitilafu baina ya nchi hizo mbili jirani zinapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa njia za amani.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Ethiopia hivi majuzi alinukuliwa akisema kuwa, Addis Ababa inataka kutatua hitilafu zake za mpaka na Sudan kwa njia za amani na haitaingia vitani kutokana na kadhia hiyo.

Dina Mufti alisema hayo kutokana na kushadidi hitilafu za mpaka kati ya Ethiopa na nchi jirani ya Sudan na kuongeza kuwa: Ni jambo lililo mbali kutokea vita baina ya pande hizi mbili katika mzozo huu wa mpaka. 

Wasiwasi katika mpaka wa Sudan na Ethiopia uliongezeka baada ya kutokea mapigano katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka jana.

Mzozo baina ya Sudan na Ethiopia unahusiana na maeneo ya kilimo katika eneo la al Fushqa hasa baada ya wakulima kutoka Ethiopia kuyavamia maeneo hayo ya Sudan.

Hivi karibuni kuliripotiwa kutokea mapigano ya silaha baina ya wanajeshi wa Sudan na Ethiopia huku kila upande ukiushutumu upande mwingine kuwa ndio ulioanzisha mapigano hayo.