Pigo kubwa waumini wa dini, Wasema hakuwa mbaguzi

Alimtanguliza Mungu mbele kwa kila jambo

NA MWANTANGA AME

NI Jumatano ya tarehe 17 mwaka huu, ambayo haitasahaulika vichwani mwa watanzania kwa kupokea taarifa za msiba wa Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli.

Taarifa iliyotolewa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, sasa ni rais baada ya kula kiapo cha wadhifa huu siku mbili baada ya kifo cha Dk Magufuli.

Taarifa hiyo ilikuwa kama hivi ifuatavyo :-

“Ndugu wananchi kwa masikitiko makubwa, nawajulisha kuwa leo tarehe 17 Machi mwaka huu wa 2021 majira ya saa 12 jioni tumempoteza kiongozi wetu shupavu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ambaye amefariki kwa maradhi ya moyo katika hospitali ya Mzena jijini Dar es salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mheshimiwa Rasi Magufuli alilazwa tarehe 6 machi mwaka huu katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete kwa tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10.

 Aliruhusiwa tarehe 7 Machi mwaka huu na kuendelea na majukumu yake. Tarehe 14 Machi mwaka huu alijisikia vibaya na kukimbizwa hospitali ya Mzena ambako aliendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete hadi umauti ulipomkuta.

Mipango ya mazishi inapangwa na mtajulishwa. Nchi yetu itakuwa kwenye maombolezo kwa siku 14 na bendera zitapepea nusu mlingoti.”

Hilo lilikuwa ni tangazo la serikali lilitolewa na Makamu wa Rais ambaye hivi sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samiha Suluhu Hassan.

Taarifa hizo ambazo zilianza kusambaa tokea usiku wa saa tano, lakini wazanzibari wengi wamepata taarifa hizo asubuhi huku baadhi ya shughuli za serikali zikiakhirishwa na watu kujikusanya kwa makundi kuzungumzia suala hilo.

Ni dhahiri kuwa Rais Magufuli, alikuwa ni kipenzi wa watu kwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ilijigubika na watu kujaa nyuso za simanzi.

Watu walizungumza kwa hisia za kumpoteza kiongozi huyo na kusema kwamba ameacha pengo kubwa kwa siasa za Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono maridhiano ya Zanzibar na ujasiri wake wa kuongoza nchi.

Kwa kuwa kiongozi huyo hakuwa mbaguzi wa dini, kabila, chama wala mahala alipotoka mtu, basi kwa upande wao Viongozi wa dini walisikitishwa sana na msiba huo na kueleza kwamba hawatausahau mchango wa Magufuli katika kuinua misingi ya dini bila ya ubaguzi katika uongozi wa nchi.

Walisema alishirikisha viongozi wa dini, katika shughuli zake zote bila ya kufanya ubaguzi kwa kuwa madhehebu yote yaliunguna katika shughuli za kijamii, kisiasa kiuchumi na kimaendeleo kiasi ambacho walijisikia kwamba Magufuli hakuwa ana upendeleo katika mambo ya dini.

Aidha Magufuli katika uhai wake aliwahi kusema viongozi wa dini wanafanya kazi kubwa ya kuhubiri amani, umoja na mshikamno, hivyo Watanzania wana kila sababu ya kuwaunga mkono.

Alisema kwamba viongozi wa dini wanafanya kazi kubwa na muhimu katika Taifa na kwamba Watanzania wote bila kujali dini zao, itikadi za kisiasa, makundi na kanda zao wana wajibu wa kuungana na viongozi hao ili nia hiyo njema iendelee kufanikiwa.

Ndio maana leo hii viongozi hao wa dini wanaungana na watanzania kuomboleza kifo hicho, kwani wanaona thamani waliyoipata katika kuchangia Amani na utulivu uliopo nchini.

Vile vile, Dk. Magufuli katika kupambania dini alifanya jambo kubwa la kufanikisha ujenzi katika nyumba za ibada kwani alijitolea kufanya harambee za ujenzi wa misikiti pamoja na makanisa huku akiomba misaada ya ujenzi huo.

Mfano wa hilo Agosti 23, 2020 katika Misa Takatifu na uzinduzi wa Kanisa, Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma, Rais Pombe Magufuli, aliendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa Msikiti wa Chamwino ambapo alifanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 48 ziliipatikana pamoja na ahadi za vifaa vya Ujenzi.

Harambee hiyo yenye lengo la kuhakikisha Makao Makuu ya nchi yanakuwa ni sehemu ambayo imezungukwa na uwepo wa Mungu, na kueleza kuwa Msikiti wa Chamwino bado ni mdogo hivyo ipo haja ya kuchangia ili uweze kuwa mkubwa.

Moja ya neno lake alilolisema … “Mahali ambapo ni Makao Makuu ni lazima pazungukwe na watu wanaomtukuza Mungu, Baba Askofu kama utaniruhusu na hili nakuomba sana, basi tutumie siku ya leo pia tuchange tuanze kujenga Msikiti wa ndugu zetu Waislamu ambao Msikiti wao ni mdogo na wapo pale kwa ajili ya kumtukuza Mungu na baadhi ya wasaidizi wangu ni Waislamu na yupo anaitwa Alhaji na ameshaenda kuhiji”,  mwisho wa kumnukuu.

Sheikh Suleiman Machano, alisema kifo cha Magufuli, kimewapa mshutuko mkubwa kwani wamepoteza kiongozi mzuri ambaye aliwapambania waumini wake bila ya ubaguzi wa kidini.

Alisema hiyo ni kutokana na kwamba katika uhai wake alionyesha Imani ya dini ilikuwa kubwa katika nafsi yake kiasi ambacho katika mikutano yake yote aliyokuwa akiifanya aliwashirikisha viongozi wa dini tofauti kwa kuruhusu kuombewa dua taifa ama mradi anaoufungua.

ALIYEKUWA Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Dkt. John Pombe Magufuli akimzawadia Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kiislamu ya Amana Dr. Muhsin Salim Masoud ambapo Benki hiyo ndiyo ilikuwa wadhamini wakuu wa mashindano maalumu ya 2o ya Qur’aan Tukufu yaliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam hapo Mei 19, 2019.

Sheikh Suleiman, anasema katika uhai wake ameendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa misikiti huku wachungaji wa madhehebu mbalimbali wakishiriki shughuli hiyo.

“Magufuli aliwafanya viongozi wa dini kuwa wamoja kwani aliwakutanisha pamoja katika kamati za usalama na Amani ambazo zilikuwa na viongozi wa dini wa madhehebu yote” alisema.

Amesema katika jambo kubwa watalomkumbuka ni pale Rais Magufuli, alipoonesha kujali maendeleo ya waislamu alipofanya ziara ya kushtukiza ili kukagua maendeleo ya ujenzi wa Msikiti wa BAKWATA unaojengwa eneo la Kinondoni, Dar es Salaam, kwa ufadhili wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Al had Salim Mussa anasema kwamba kifo cha Magufuli kimeacha pengo kubwa kwa wananchi wa Tanzania na hawataweza kusahau katika mchango wake alioutoa katika kuinua dini zote nchini kwani amewakuwa akishirikiana na madhehebu yote.

Sheikh Mussa Salim alisema waumini wa kiislamu kote nchini waendelee kusimmia Amani kama msingi bora aliowaachia marehemu Magufuli kwani katika kazi zake zote alihimiza hilo.

Aliwataka watanzania kuendelea kumtukuza Mwenyezi mungu, huku wakijawa na subira kutokana na kifo hicho, kwani kila mja atapitia njia hiyo.

Nae Askofu wa Kanisa Anglican Zanzibar, Michael Hafidhi, alisema kifo cha Magufuli kimewapa mshutuko mkubwa na hakuna budi kumuombea na kuenzi yale aliyoyaacha.

“Ametuachia nchi ikiwa na amani, utulivu na upendo kwani alikuwa ni mtu wa Imani katika kuendesha nchi yetu, mpenda wananchi wake na alitaka nchi hii kuiweka katika ramani ya kimatifa kutokana kila anapokutana na viongozi wa dini alituhimiza tuhubiri amani”, alisema.

“Hivi ni juhudi kubwa alizozifanya katika kipindi chake cha urais alipenda maendeleo lakini Mungu amemchukua hatuna la kufanya, ila tukubali matokeo kwa kuendelea kudumisha amani ya nchi kwa kuwaunga mkono viongozi waliopo  tuijenge Tanzania yetu”, alisema Michael.

Alisema kinachohitajika hivi sasa ni kuona viongozi waliopo serikali wanaendeleza malengo aliyoyaanza pamoja na kuhakikisha taifa haliyumbi ili wananchi waendelelee kufanya ibada zao bila ya bughuda ikiwa ni pamoja na kuiombea dua nchi iendelee kuwa na amani, mshikamano, umoja pamoja na kuendelea kuchapa kazi kwa maslahi mapana ya nchi.

“Kuna mafunzo Fulani tunayapata katika uongozi wake, tunahitaji kuyafuata ili tuwe viongozi bora hatuwezi kukataa hilo hususan katika mambo ya haki hasa kwa watu wanyonge kwani Magufuli aliweza kutoa maamuzi hapo hapo na kuleta tija hilo ni jambo zuri alilokuwa nalo”, alisema.

Alisema katika Mtazamo wa kidini binadamu wapo duniani kwa muda na hilo wanatakiwa kujua kuona leo wapo na kesho wataondoka jambo ambalo wanahitaji kujipanga ili kuona watapoondoka watakumbukwa huku wakijenga dhana hata wasipokuwepo watakuja watu wengine.

Alisema Tanzania bado iko imara na wanachi wanatakiwa kuondoa hofu kama nchi itayumba kwani bado Mungu yupo kwa vile hata Marehemu Magufuli, alikuwa akiwahamasisha siku zote kumtanguliza Mungu mbele katika kila jambo kwani bado yupo.

Kutokana na hali hiyo inaonesha dhahiri kuwa mchango wa Magufuli katika dini hautasahaulika kwa kuwa aliwaunganisha watu wote katika kila nyanja.