HATUNAYE na hatutakuwa naye tena katika maisha ya duniani tuliyoyazoea, kifo kimemtenganisha Dk. John Pombe Magufuli na familia, ndugu, jamaa na wananchi wote wa Tanzania aliokuwa akiwaongoza kwa mapenzi makubwa.

Mafundisho ya kiimani yanatuelezea kuwa kiongozi wetu huyo wa awamu ya tano wa Tanzania atakwenda kuanza maisha mengine mpya na ya milele baada ya muda maalum wa uhai wake kumalizika hapa ulimwenguni.

Watanzania wakati huu tukiwa kwenye maombolezo ya Dk. John Pombe Magufuli, pamoja na kuhuzunishwa na kifo hicho, lakini tukumbuke kuwa mauti ni mlango na kila mtu atapita pia mauti ni kinywaji kila mmoja atakunywa.

Dk. Magufuli alifariki kutokana na ugonjwa wa moyo na kwamba alilazwa katika hospitali ya Mzena iliyopo jiji Dar es Salaam huku mataktari wakimpatia matibabu na uangalizi maalum, hata hivyo siku ikifika haina dawa, hakuna kukata rufaa wala hakuna kafara.

Pamoja na kwamba kwa wakati huu tukiwa na majonzi na simanzi kwa kuondokewa na kiongozi wetu huo, hatuna budi tukubaliane na uwezo wa Mungu ambaye amempenda zaidi na bila shaka amemuondosha duniani ili atupe mtihani.

Hapana shaka yapo mengi katika utawala wa miaka mitano na kidogo wa Dk. John Magufuli yatakayoandikwa katika kurasa za historia, hasa yale mazuri aliyoyafanya kwa maslahi ya watanzania.

Magufuli alikuwa kiongozi mwenye msimamo asiyeyumba katika kutekeleza yale aliyoyaamini kuwa yana faida na tija kwa wananchi wa Tanzania, kwa hakika sifa hiyo ilimuwezesha kumudu vyema kutekeleza majukumu yake.

Watanzania watamkumbuka marehemu kama kiongozi aliyesimama kupinga vitendo vya rushwa, sio kwa maneno matupu, bali alichukia kwa dhati vitendo hivyo na kuwawajibisha wale waliokuwa wakituhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo.

Hakuwa rais wa kuchezewa wala kujaribiwa na wale waliomjaribu aliwanyoosha na hivi ndivyo inavyotakiwa hasa ikizingatiwa kuwa wakati mwengine ukiwa mpole sana wapo wengine hupenda kukuchezea na kukujaribu.

Kwa hulka yake alisimamia kila mradi ambao ulitumia fedha za umma, hali hii ilisaidia miradi mingi na mkubwa kujengwa kwa kiwango, kwa wakati na kuzingatiwa matumizi ya fedha za umma.

Katika uongozi wake Dk. John Pombe Magufuli, alijipambanua kama kiongozi aliyewajali na kusimamia haki za wanyonge ambao ndio tabaka kubwa la watanzania na ndilo tabaka la uzalishaji na ujenzi wa uchumi wa nchi.

Magufuli wakati anachukua uongozi Tanzania aliikuta nchi ambayo mifumo ya kiutendaji imevurugika, huku kazi zikizongana hajulikani nani anafanya nini na nani anawajibika wapi.

Hili alilipatia ufumbuzi kwani alizipa mamlaka za kiutendaji nguvu na meno ya kuhakikisha zinafanyakazi kwa mujibu wa sheria pasi na kuingiliwa wala kuogopa.

Hapana shaka Dk. John Magufuli alikuwa kiongozi anayefaa katika Tanzania ya sasa na tungependa tuendelee kuwa naye kwa miaka mingi ijayo, lakini hatuwezi kushindana na uwezo wa Mwenyezi Mungu ambaye amemuhitaji.

Wakati tukiomboleza kifo cha Dk. Magufuli lazima tuyaendeleze mazuri aliyoyaasisi na kwamwe tusikubali kurudi nyuma ama kuwaruhusu wachache kwa maslahi yao waturejeshe nyuma.

Itakuwa kosa kubwa Tanzania baada ya Magufuli kurejea kwenye kurasa za madaftari ya mashirika ya kimataifa kuwa ni miongoni mwa nchi masikini sana, wakati mwaka jana kiongozi huo aliinua nchi kufikia taifa lenye kipato cha kati.

Magufuli amekuwa sehemu ya watu walioishi duniani na kuandika historia inayosimuliwa kwa mazunri mengi, tanadhani hii ni fursa ya viongozi waliopo nao kujitathmini wakiondoka watazungumzwa vipi?

Buriyani Dk. Magufuli, kwaheri ya kuonana, mchango wako kwa Tanzania utaandikwa kwa wino wa dhahabu na kwamba daima hautafutika wala kuchakaa.