TEL AVIV, ISRAEL

WANAJESHI wa Israel wamempiga risasi na kumuuwa raia mmoja wa Palestina, aliyekuwa akishiriki maandamano kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kimabavu na Israel hapo jana.

Wizara ya Afya ya Palestina ilisema mtu huyo alipigwa risasi ya kichwa katika kijiji cha Beit Dajan, karibu na Nablus.

Meya wa Beit Dajan, Abdelrahman Hanani, alisema Atef Yussef Hanaysheh, mwenye umri wa miaka 42 alipigwa risasi akiwa kwenye maandamano ya kupinga ujenzi wa makaazi ya walowezi.

Mamia ya Wapalestina walikusanyika hapo jana kuandamana dhidi ya utanuzi wa makaazi hayo ya walowezi, ambao unatambuliwa kuwa ni haramu kwa sheria za kimataifa.

Mbali ya wale wanaoishi kwenye makaazi ya walowezi ya mashariki ya Jerusalem, walowezi wengine 450,000 wa Kiisraeli wanaishi kwenye Ukingo wa Magharibi, eneo ambako wanaishi Wapalestina milioni 2.8.