CAIRO, MISRI
TAKRIBAN watu 11 wamefariki na wengine 98 walijeruhiwa katika ajali ya treni iliyotokea siku ya Jumapili katika mji wa Delta wa Toukh, kaskazini mwa mji mkuu wa Misri Cairo, Wizara ya Afya ya Misri ilisema.
Taarifa hizo ziliongeza kuwa jumla ya magari ya wagonjwa 60 yamepelekwa eneo la tukio na waliojeruhiwa wamehamishiwa katika hospitali tatu za umma, ilisema wizara hiyo katika taarifa.
Ajali hiyo ilitokea baada ya mabehewa manne ya gari moshi, kutoka Cairo kwenda mji wa Delta wa Mansoura, kuacha njia, Wizara ya Uchukuzi ya Misri ilisema.
Rais Abdel-Fattah al-Sisi ameamuru kuundwa kwa kamati itakayowasilisha ripoti kuhusu sababu za ajali hiyo.
Uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea na dereva wa treni na msaidizi wake, na maafisa wengine wanane katika kituo cha treni cha Toukh, ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Umma ilisema.
Misri imekuwa ikishuhudia ajali za mara kwa mara za treni. Mapema wiki iliyopita, watu 15 walijeruhiwa baada ya treni nyengine kuacha njia katika jimbo la kaskazini la Minya al-Qamh.
Aidha Tarehe 26 Machi, treni mbili za abiria ziligongana kusini mwa nchi hiyo na kuuwa watu 19. Mwezi Februari 2019, ajali ya treni ilisababisha vifo vya watu 31.M