NA MARYAM HASSAN
RAIA wa Romania aliyesababisha kifo cha mfanyakazi wa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Khamis Ali Khamis, amemusurika kwenda jela baada ya kulipa faini aliyotozwa katika mahakama ya mkoa Mwera.
Farima Feras(24) akiwa na mwenzake Vuaa Masoud Hassan (26) wote ni wakaazi wa Jambiani, walifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Khamis Ali Simai, kujibu tuhuma hizo.
Kwa pamoja, wadaiwa kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha kifo, kinyume na kifungu cha 115 (1) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.
Hakimu huyo, aliwataka kila mmoja kulipa faini ya shilingi 1,500,000 kwa kosa la kwanza na kosa la pili walitakiwa walipe shilingi 500,000 wakishindwa watumikie Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka mitatu.
Mapema, wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Sara Omar Hafidh, alidai kuwa kosa hilo walitenda Machi 10 mwaka huu majira ya saa 3:30 za asubuhi, huko Kitogani wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.
Wote kwa pamoja, wakiwa ni dereva wa gari yenye nambari za usajili Z 178 KT na gari Z 511 KG wakati wakitokea Paje kuelekea Kitogani, walipofika maeneo hayo karibu na kambi ya Zimamoto waliendesha gari hiyo kwa uzembe na kupelekea ajali iliyosababisha kifo cha Khamis Ali Khamis, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Kosala pili ni kuingilia msafara wa kiongozi, kinyume na kifungu cha 128 (a) (1)cha sheria nambari 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar
Siku hiyo hiyo, wanadaiwa kuingilia msafara wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Waliposomewa makosa hayo washitakiwa hao walikubali na kuiomba mahakama kuwapunguzia adhabu, kwa sababu kosa walilofanya hawakufanya makusudi.
Baada ya kupewa adhabu hiyo, washitakiwa hao walilipa ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka mitatu.