NA MARYAM HASSAN

BAADA ya kuona shauri lake lipo mahakamani kwa muda mrefu, mshitakiwa Abdulkadir Mohammed Said (28) mkaazi wa Michamvi, ameiomba mahakama kumuondolea shitaka lake.

Mshitakiwa huyo alitoa kauli huyo mbele ya Hakimu Said Hemed Khalfan wa mahakama ya mkoa Mwera.

Alisema ni muda mrefu upande wa mashitaka hauwasilishi mashahidi na kila siku wanaeleza kuwa hawajapokea, hivyo amesema ni vyema mahakama ikazingatia ombi lake.

Wakati anaeleza hayo, upande wa mashitaka uliokuwa ukisimamiwa na wakili wa Serikali, kitoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ayoub Nassor Sharif.

Mapema wakili huyo aliiambia mahakama kuwa, hawajapokea shahidi na kuomba kuahirishwa shauri hilo.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu huyo aliahirisha shauri hilo na kupangwa kusikilizwa tena Aprili 8 mwaka huu.

Aidha Hakimu huyo aliwapa onyo ya mwisho upande wa mashitaka, kwambia endapo hawatoleta shahidi kikao kinachofuata mahakama itatoa maamuzi yanayofaa.

Mshitakiwa alifikishwa mahakamani kwa kosa la shambulio la hatari, alilodaiwa kutenda Oktoba 12 mwaka 2019 majira ya saa 4:00 za usiku, huko Michamvi Pongwe wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa anadaiwa kumshambulia kwa hatari Aisha Shaaban Hussein, kwa kumpiga panga sehemu ya kichwa na kumsababishia maumivu makali mwilini mwake, jambo ambalo ni kosa kisheria.