Amebatizwa jina la ‘Amina Mzanzibari’ nchini Australia
Awashauri wazazi kuwaruhusu vijana kufanyakazi ya ubunifu mavazi
NA ABOUD MAHMOUD
“NAJISKIA fahari tena najivunia kuzaliwa Mzanzibari, hivi sasa sehemu mbali mbali ninazokwenda za nje ya nchi hususan Australia ambapo ndio ninapoishi najulikana kwa jina la Amina Mzanzibari na nikiitwa hivyo hujisikia furaha na najivunia na kuitangaza nchi yangu”.
Hayo ni maneno ya mbunifu wa mavazi ambae pia ni muigizaji wa filamu nchini Australia mzaliwa wa Zanzibar, Amina Bilal Pira.

Amina amejikita katika kufanya kazi hizo za ubunifu wa mavazi na kusaidia katika kutangaza vyema kazi yake hiyo pamoja kuutangaza utamaduni wa Zanzibar kupitia mavazi anayoyabuni akiwa nchini Australia.
Mwandishi wa makala hii alifika katika mtaa wa Shangani kwenye duka la mbunifu huyo na kuzungumzia naye kwa kina mambo mbali mbali ya kazi zake hizo alipoanzia, alipofikia na matumaini yake ya baadae.
Amina kwa umbile la nje ana umbo la wastani ni mrefu mwenye rangi ya maji ya kunde, mcheshi na mzungumzaji kwa watu wa rika tofauti kwani unapofika kwake hata kama hakujui hukupokea uzuri na tabasamu la hali ya juu huku akikukaribisha na kuzungumza nae kama mtu mnayejuana miaka mingi.

Kuhusu kujikita katika fani hiyo, mbunifu huyo wa mavazi, alisema, alianza kazi hiyo akiwa mdogo kwani alijifundisha kushona kutoka kwa mama yake mzazi ambaye alikuwa mshoni mahiri na yeye alijifunza na mwisho aliweza na akawa anashona nguo mbali mbali ikiwemo sare za skuli, mahoteli, mashuka na mapazia.
Lakini, alisema, akiwa anajishughulisha na ushonaji wa nguo, hamu yake ilikua katika urembo na kuonesha mavazi kwa jina la siku hizi mwanamitindo.

“Nilikua napenda mambo ya wanamitindo na nashukuru kwa miaka hiyo kulikuwepo na maonyesho ya mavazi na mimi nilishikiri na nilibahatika kutwaa mataji ya ‘Miss Kwerekwe’, na baadae nikaingia katika mashindano ya ‘Miss Bwawani’ na nikapata nafasi ya kuwa mshindi wa tatu”, alisema.
Baada ya hapo, Amina, alisema alibahatika kuolewa na kundoka visiwani Zanzibar na kwenda kuishi nchini Australia katika mji wa Quensland Brisbane ambapo alipofika huko aliachana na shughuli zote kutokana na kuwa mgeni katika nchi hiyo pamoja na uzazi na ulezi wa watoto wake ulimfanya aachane na shughuli hizo.
“Baada ya kufika Australia pirika zangu zote zilisimama kwa sababu kwanza nilikua mgeni halafu pia nilifika alhamdulilah nikajaaliwa kupata watoto kwa hiyo nilishindwa kufanya lolote”.

“Lakini baadae nilipoona watoto wangu washaanza kukua nikaingia mitamboni kurudia kazi zangu za kushona,”alisema.
Mbunifu huyo, alisema, alianza kufanya maonyesho ya nguo za asili ya Zanzibar ambapo ndipo alipobatizwa jina la Amina Mzanzibari na watu wa mataifa mbali mbali wakiwemo wenyeji wa Australia kupenda nguo hizo na kumtaka awashonee.
“Nilianza kufanya ‘Traditional Swahili Night’ na nilikua nashona nguo zenye asili ya nyumbani na watu wengi walikua wanapenda, hapo ndipo akili yangu ikazidi kufunuka na nikawa nakwenda katika miji mbali mbali kwenye masoko kutangaza kazi zangu”, alisema
Alisema, kutokana na mafanikio aliyoyapata katika kutangaza kazi yake ya ubunifu wa mavazi, alifanikiwa kufungua duka lake ambalo alilipa jina la TUNTUFADY ni herufi zinazotokana na majina ya watoto wake.
Akili ya kuwa mbunifu bora na maarufu ilionekana kutawala kwenye kichwa cha Amina ambapo mara baada ya kufungua duka hilo, alijipatia umaarufu zaidi na kuanza kufanya maonyesho katika miji mbali mbali nchini humo .
“Niliweza kuutangaza vyema Uzanzibari kupitia mavazi yetu ya asili, lakini pia niliwahi kufanya mashindano ya ‘Miss Brisbane pamoja na kuwavalisha warembo wengi nchini humo”, aliongezea.
Mbunifu huyo, alisema, akiwa anajishirikisha kwake katika fani hiyo na uanamitindo kipindi hicho akiwa hajaolewa hakupata kikwazo kutoka kwa wazee wake kutokana na walikua wanajua nini anachokifanya.
“Changamoto niliyoipata ilikuwa kwa watoto wangu wakati huo wadogo na mimi nataka kufanya kazi zangu, ikanibidi nisite nilee kwanza na baada ya kukua nikaendelea na kazi kwa hiyo haikua changamoto kubwa ya kunisumbua akili yangu,”alisema.
Kuhusu faida, alisema, zipo nyingi ikiwemo kuitangaza nchi yake kimataifa, kuweka lebo ya kazi yake, umaarufu, kushirikiana na jamii lakini pia kufanikiwa kujenga nyumba ya kuishi Zanzibar na Australia.
Amina ni mama mwenye familia ya watoto wanne, watatu wanawake na mmoja mwanamme, anasema, katika watoto wake hao mwanawe wa kwanza aliyemtaja kwa jina la Zaitun amemrithi mama yake katika kazi yake hiyo ya ubunivu. Zaitun amemaliza masomo ya ubunivu wa mambo mbali mbali.
“Huyu amerithi nyayo zangu na amewahi kuwa mrembo wa Afrika nchini Australia. Yeye ndiye ananisaidia katika mambo mbali mbali yanayohusiana na ubunifu,”aliongezea.
Aidha, alisema, akiwa nchini Australia alijiunga na chuo maarufu kinachojulikana kwa jina la ‘Image Management Gold Cost Australia’ kwa ajili ya kujifunza uigizaji.
Alisema baada ya kumaliza masomo hayo, alifanikiwa kushiriki katika filamu mbali mbali akiwa na waigizaji maarufu na kulitangaza jina lake katika eneo jengine la sanaa ya filamu.
“Nashkuru sikuishia kwenye ubunivu wa mavazi, niliamua niingie kwenye filamu, napenda kuigiza na niliwahi kuigiza miaka hiyo katika kipindi kilichokua kinaitwa ‘Shangazi na wanawe’, kilikua kinaonesha na TVZ”, alisema.
Alizitaja filamu alizoigiza ni pamoja na ‘San Andreas’, filamu iliyomshirikisha muigizaji maarufu duniani Dwayne Johnson, Pirates of Carribien, Aqua Man,Jerra Nova ambazo zote alizifanya nchini Australia akishirikiana na waigizaji maaarufu nchini humo na duniani kwa ujumla.
Pia akiwa nchini Australia, msanii huyo aliigiza filamu inayojulikana kwa jina la ‘Mkono mtupu’ ambayo iliigizwa kwa kutumia lugha ya Kiswahili iliyoongozwa na msanii maarufu nchini Tanzania, Daud Michael ‘Duma’ na hivi sasa pia ameshiriki katika filamu ya ‘Vuta nikuvute’ ambayo bado haijatoka.
Alisema, anapendelea na anatamani kuwavalisha watu maaarufu kama vile wasanii wa nchini Marekani akiwemo Beyonce na wake wa viongozi mbali mbali duniani ili kuutangaza utamaduni wa Zanzibar.
“Natamani nifikie huko, lakini, pia natamani ili ndoto zangu zikamilike niwe kama marehemu mama yangu ambae alikuwa mbunifu mkubwa wa mavazi hapa nyumbani na aliwashonea wake wa viongozi wengi nchini.
“Lakini pia mama ndiye alieshona sare za skuli za wanafunzi wa msingi wa mwanzo baada ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar”, alisema.
Mbunifu huyo wa mavazi na muigizaji alitoa wito kwa wananchi kulinda mila na tamaduni za Zanzibar kwa kuvaa mavazi ambayo yanaendana na utamaduni wa nchi ili kuitangaza kitaifa na kimataifa.
Pia aliwashauri wazazi kuwarhusu vijana wao kushiriki ubunifu wa mavazi ambapo alisema kwamba ni moja ya kazi kama kazi nyengine na kukanusha kwamba kazi hiyo sio uhuni .
Amina Bilal Pira amezaliwa Oktoba 9 mwaka 1968 akiwa mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne, watatu wanawake na mmoja mwanamme.
Elimu yake alianza mwaka 1975 katika Skuli ya Wete, Pemba na baadae aliendelea na masomo katika Sekondari ya Kengeja na baada ya baba yake kurudishwa kikazi Unguja, aliendelea na masomo yake Skuli ya Kiponda na kumalizia elimu yake ya kidato cha nne Lumumba.
Baadaye alijiunga na Chuo cha Uchumi kujifunza uchapaji ambacho hivi sasa kinajulikana kwa jina la Chuo cha Utawala wa Umma (IPA).