NA KHAMISUU ABDALLAH
BAADA ya mahakama kutaka kusoma hukumu kwa mshitakiwa Salum Omar Salum (31) mkaazi wa Mtoni Kidato wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, hatimae mshitakiwa huyo aliomba mahakama kumpunguzia adhabu.
“Mheshimiwa Hakimu naomba mahakama yako inipunguzie adhabu kwa sababu nna wake watatu na watoto tisa na mzee wangu ni mgonjwa wa sukari na mimi ndie nnaemuhudumia”, aliiomba.
Hakimu Suleiman Jecha Zidi wa mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe, alisema mahakama imezingatia ombi la mshitakiwa na kumtaka kulipa faini ya shilingi 150,000 au kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi miwili.
Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda jela kwa muda huo.
Salum, alipewa hukumu hiyo na mahakama baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kufanya kitendo kinachoashiria uvunjifu wa amani, kinyume na kifungu cha 73 (1) (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.
Alidaiwa kuwa, Machi 18 mwaka 2020 saa 2:30 usiku huko Mtoni Kidato, alitoa lugha za matusi kwa Ali Issa Hamad kwa kumwambia mshirikina, paka mweusi na amemuua baba yake, kitendo ambacho kingesababisha uvunjifu wa amani na ni kosa kisheria.
Mshitakiwa huyo baada ya kusomea shitaka hilo kwa mara ya kwanza Disemba 7 mwaka jana na Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Salum Ali alilikataa, ndipo upande wa mashitaka ulipodai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika, jumla ya mashahidi watatu walitoa ushahidi wao mahakamani hapo.
Hakimu Suleiman, alitoa hukumu hiyo Machi 19 mwaka huu na kutoa haki ya rufaa kwa siku 30 kwa mtu asieridhika na hukumu hiyo.