WASHINGTON, MAREKANI

MAELFU ya watu nchini Marekani, wanaendelea kushangiria hukumu ya kwanza, iliyomtia hatiani afisa polisi wa kizungu, kwa mauaji ya mtu mweusi, katika historia ya taifa hilo. Hata hivyo, Rais Joe Biden alisema kutiwa hatiani kwa Derek Chauvin, kwa mauaji ya George Floyd, kunaweza kuwa hatua kubwa, katika vita dhidi ya ubaguzi wa kimfumo, lakini hakutoshi.

Biden aliyekuwa akizungumza katika Ikulu ya White House akiwa na makamu wake, Kamala Harris, muda mchache baada ya mahakama kumtia hatiani Chauvin, kwa mashitaka matatu ya mauaji, alisema Marekani haipaswi kutosheka na hukumu hiyo pekee, bali kusonga mbele hadi mfumo mzima, uwe umebadilishwa.

Viongozi hao wawili wamelitolea wito baraza la Congress, kuyashughulikia haraka mageuzi ya polisi, ikiwemo kuidhinisha muswaada wa sheria, uliopewa jina la Floyd, aliyeuawa akiwa amegandamizwa goti shingoni, mwezi Mei mwaka jana.