NA FATMA KASSIM

BARAZA la Tiba Asili na Mbadala limefanya ukaguzi wa kushtukiza kwa wauza dawa za tiba asili na viringe, ambapo imebaini kasoro zinazoweza kusababisha madhara makubwa kwa watumiaji wa dawa hizo.

Kaimu Mrajis wa Baraza hilo Mohamed Mshenga Matano, alisema kasoro hizo ni pamoja na wauza dawa wengi wa jamii ya kimasai kuuza kiholela katika maeneo ya wazi.

Mrajis huyo alisema kuwa kasoro nyengine iliyobainika ni kutojisajili katika baraza hilo, uhifadhi usio mzuri wa dawa na dawa hizo hazioneshi tarehe iliyotengenezwa na kumaliza muda wa matumizi.

Alisema ni wajibu wa kila raia au mwananchi anaetaka kutoa huduma za tiba asili ni vyema kufika katika baraza hilo kwa ajili ya kujisajili na wale wote wanaokiuka sheria Baraza litachukua hatua.

Alisema uuzwaji wa dawa unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara umeonekana kuwa hauridhishi kutokana na dawa hizo mara nyingi zinatumiwa kwa kunywa na kupelekea madhara makubwa kwa watumiaji.

Mrajis huyo alifahamisha kuwa licha ya kutolewa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa za miti shamba bado jamii inaona dawa hizo hazina madhara kutokana na dawa nyingi zinatokana na mimea ya asili pamoja na miti shamba.

Alisema tafiti mbalimbali zilizofanywa zimebainisha kuwa baadhi ya dawa asili zina vinasaba vyenye sumu ambavyo vinasababisha madhara kiafya.

Aidha alisema jitihada mbali mbali zimefanyika ikiwemo kuchukua sampuli za tumbaku ya ugoro kwa kufanyiwa uchunguzi katika maabara ya Wakala wa Chakula na Dawa na kubainika kutiwa unga wa betri katika baadhi ya tumbaku ya ugoro.

Aliwataka wananchi kutotumia dawa hizo kiholela ambazo zinasababisha madhara makubwa na athari zake hazitokezi mara moja na zinaweza kuchukua muda mrefu.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Mbadala, Habib Ali Sharif alisema wananchi wengi wa Zanzibar wana tabia ya kutofuata taratibu na kununua dawa sehemu zisizo rasmi ambazo hazina ubora wa matumizi ya mwanadamu.

Alifahamisha kuwa lengo la Baraza hilo si kuwanyanyasa wauzaji wa dawa hizo bali ni kuhakikisha wananchi wanapata tiba iliyokuwa sahihi na sio kumdhuru mtu.

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano mkubwa kwa baraza hilo wakiona dawa zinauzwa katika maeneo yasiokuwa rasmi  pamoja ikiwemo masokoni na maeneo ya wazi.