Changamoto zatatuliwa hatua kwa hatua
NA MWANDISHI WETU
SIKU kama ya leo Jamhuri ya Zanzibar na ile ya Tanganyika kwa pamoja ziliungana na kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo iliasisiwa na waasisi wetu Mzee Abeid Amani Karume na Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Kila ifikapo tarehe 26 Aprili wananchi wa visiwani na wa Tanzania bara, wanasherehekea siku hii adhimu kwa kuwafanya kuwa wamoja huku wakizidi kuimarisha muungano huu ambao ni wa mfano barani Afrika na dunia kwa ujumla.
Ni wazi kuwa miaka 57 ya muungano wa Tanzania, pamoja na changamoto zilizopo lakini kuna mambo kadhaa ambayo yamepiga hatua kubwa baina ya nchi mbili hizi jambo ambalo linazidi kuimarisha muungano huu.
Basi katika makala haya tutangalia namna ya changamoto na mafanikio ya kibiashara katika muktaza wa muungano.
Kwa mfano ushirikiano kati ya taasisi ya viwango Zanzibar (ZBS na ile ya shirika la viwango Tanzania (TBS) zinaendelea kushirikiana kwa karibu kupitia utekelezaji wa hati ya ushirikiano.
“Memorandum understanding” (MoU) kati ya TBS na ZBS ilizinduliwa Mei 4, 2015 na aliyekuwa waziri wa viwanda, Biashara na Uwekezaji, Abdalla Kigoda na pia aliekuwa waziri wa viwanda na Masoko Zanzibar, Nassor Mazrui”, kwa mujibu wa taarifa wa iliyokuwa wizara ya Biashara na Viwanda.
Ushirikiano huo uliopo unaendelea kuimarika hasa katika uandaaji wa mambo yanayohusu ubora wa bidhaa kwa lengo la kulinda soko la nchi na ustawishaji wa bidhaa.
Kuhusiana na hati ya makubaliano, taarifa hiyo iliongeza kuwa ni pamoja na ushirikiano katika misaada ya kiufundi hasa katika utengenezaji wa bidhaa sambamba na ubunifu wa mifumo inayohusiana na viwango vya ubora wa bidhaa.
Makubaliano mengine baina ya pande mbili hizo ni pamoja na ushirikiano katika matumizi ya maabara na hasa kwa mahitaji ya taasisi hizo mbili.
Aidha katika kubadilishana utaalamu na wataalamu kwa malengo ya utekelezaji ni matarajio ya taasisi mbili kwa lengo la madhumuni ya kujenga uwezo ni miongoni mwa vipaumbele vya wizara zote mbili.
Sambamba na hilo lakini taarifa hiyo, ilisema kuwa mikutano, semina, makongamano yanayohusu ubora wa viwango na mifumo yake ni mambo yanayofanywa pamoja na taasisi hizo jambo ambalo linaonesha ushirikiano mkubwa wa kiutekelezaji wa muungano katika sekta ya biashara.
VIKWAZO VYA KIBIASHARA KWA TAASISI ZA TBS NA ZBS
Kuhusu vikwazo vya kibiashara taasisi zote mbili zinatambua alama za ubora wa bidhaa kwa kila upande jambo ambalo nyingi zao zimeshafanyiwa kazi.
Hadi kufikia sasa hakuna taasisi kati ya TBS na ZBS iliyowahi kuzuia bidhaa zenye nembo ya ubora ya TBS au ya ZBS kwa bidhaa zenye alama hizo zinapoingizwa upande mmoja wapo katika Jamhuri ya muungano.
“Hapa ndipo pale unapoona umuhimu wa kuungana nchi hizi kwa sababu bidhaa zetu zinaweza kuwa katika kiwango cha moja ya taasisi”, ilisema taarifa ya wizara.
Kuhusu upande wa bidhaa zilizokaguliwa kabla ya kuingia nchini kupitia mawakala wa ukaguzi walioko nje (PVoC) ambapo taarifa ya wizara inasema inapotokea bidhaa hizo zimeingizwa nchini na baadae kusafirishwa kwenda upande mwengine iwe Tanzania bara au Zanzibar, ZBS na TBS zinawasiliana na kujiridhisha kila upande alimradi iwe imefuatwa mifumo, sheria na taratibu zilizowekwa.
USHIRIKIANO KATIKA MAENDELEO YA VIWANGO
Wizara ya Biashara na viwanda inasema ushirikiano wa muungano wa Tanzania katika bidhaa zinazozalishwa au kuingizwa nchini kutoka nje ya nchi zinapata fursa ya soko ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
“ZBS inaendelea kuasili viwango vya Tanzania, viwango hivyo hutolewa na TBS bila ya malipo kwa lengo la kurahisisha mfumo wa mwenendo wa biashara ndani ya soko la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, ilisema.
Kwa mukhtadha huo basi, hata bidhaa zinazozalishwa Zanzibar zinaweza kuingia sokoni Tanzania bara.
Sambamba na hilo, lakini taarifa hiyo inaongeza kuwa TBS na ZBS zimekuwa zikishiriki kwa pamoja katika kuwashirikisha watendaji wa taasisi hizo mbili katika maendeleo na uoanishaji wa viwango vya Afrika Mashariki.
USHIRIKI KATIKA MIKUTANO YA KIMATAIFA
Kwa upande wa ushiriki wa mikutano ya kimataifa kwa taasisi zote mbili za biashara, taarifa ilisema kuwa zimeshiriki mara kadhaa na zinaendelea kufanya hivyo katika mikutano ya kimataifa ya biashara.
Mfano wa hiloi ni kwa Shirika la viwango la Dunia (ISO) na kamisheni ya viwango vya Bidhaa za vyakula ni moja ya mikutano inayohusisha na kushiriki kwa taasisi mbili hizo.
CHANGAMOTO
Pamoja na mafanikio makubwa katika sekta ya biashara kimuungano lakini pia kuna changamoto za hapa na pale ambazo kwa kiasi fulani zinakwaza baadhi ya shughuli katika sekta hiyo.
“Changamoto kubwa iliyopo katika ushiriki wa ZBS kuchelewa au kutopatikana kwa taarifa ya mikutano ya kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki”.
“ZBS haijawahi kushiriki katika mikutano au semina za kitaaluma kupitia jumuiya ya ushirikiano ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC).
“Hali hii inaonesha kutokufahamika majukumu ya ZBS ndani ya utaratibu wa eneo hilo na hivyo kukosa fursa muhimu za kitaaluma na kiutendaji zinazopatikana kupitia SADC kama yanavyonufaika mashirika mengine ya kikanda katika jumuiya hiyo”, ilisema taarifa hiyo.
Pamoja na mambo mengine lakini pia kumekuwa na changamoto nyengine za kibiashara mbapo wafanyabiashara wanadai kutopata fursa ya ushiriki wa mikutano ya kimataifa na kimataifa sambamba na kuingiza biashara zao Tanzania bara.
Aidha mfanyabiashara mmoja ambae hakupenda kutajwa jina lake gazetini alisema kuwa ushuru wa bidhaa zinazotoka au kuingia Tanzania bara kulipa kodi zaidi ya tatu jambo ambalo linawakwaza kibashara.
“Hili ni suala la pamoja kwa bidhaa tayari umeshalipa TRA na ZRB na utitiri mwengine wakodi unatakiwa kutoa hili linaturejesha nyuma wafanyabiashara hasa wa Zanzibar”, alisema.
Pia baadhi ya wajasiriamali na wafanyabiashara wakubwa walidai kutoshirikishwa vyema katika maonesho ya kibiashara ya kimataifa au kikanda jambo ambalo pia linaleta kero katika mukhtaza wa muungano kibiashara.
Pamoja na changamoto hizo, lakini ni wazi kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar, umeleta tija kubwa pande zote mbili kiasi kwamba ni wa kupigiwa mfano au hata wa kuonewa choyo kwa wale wasipenda amani na maendelo kwa ujumla.
Leo hii ni mafanikio mengi kama yanavyoonekana katika makala haya kuliko changamoto za kibiashara ndani ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa mantiki hiyo basi, ipo haja ya kuulinda , kuuimarisha na kuutukuza muungano wetu kwa maslahi ya maendeleo ya nchi yetu.
Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa sasa inatimiza miaka 57 huku serikali zote mbili zikitatua kero za muungano hatua kwa hatua kwa maendeleo ya wanachi wa pande zote mbili.