NA MWANDISHI WETU

HATIMAYE wajimbe 1876 wa mkutano mkuu maalumu wa CCM, wanatarajiwa kupiga kura jina moja litakalowasilishwa katika mkutano huo kumchagua mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Mkutano huo unafanyika baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais wa awamu ya tano, hayati Dk. John Magufuli kufariki dunia Machi 17 mwaka huu katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.

Kwa utamaduni wa chama hicho kuna uwezekano mkubwa jina la Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Rais wa awamu ya sita kukabidhiwa pia kofisa ya uwenyekiti wa chama jambo ambalo litarahisisha utekelezaji wa majukumu yake.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, amesema wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania wamewasili mjini Dodoma tayari kwa mkutano huo.

Alisema mbali na wajumbe hao ambao watashiriki kupiga kura, wapo wageni 1,000 watakaoshiriki mkutano wakiwamo kutoka vyama mbali mbali vya siasa nchini, wawakilishi wa vyama rafiki vilivyoshiriki katika ukombozi wa bara la Afrika na mabalozi.

Alibainisha kuwa mkutano huo utaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara, Philip Mangula na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Alisema kikao hicho kitatoa mwelekeo wa taifa kisera kwani itatolewa hutuba ya mwenyekiti mpya wa chama hicho atakayechaguliwa kuchukua nafasi ya Magufuli.

Polepole alisema, kikao hicho cha mkutano mkuu maalumu chenye jukumu la kupigia kura jina moja litakalowasilishwa ili kumpata mwenyekiti, kinakutana baada kikao cha halmashauri kuu ya CCM kukaa jana jijini kwa ajili ya kuandaa ajenda za mkutano mkuu maalumu.

Mwenyekiti mpya atakayechaguliwa anatarajiwa kupendekeza jina la Katibu mkuu wa Chama hicho kufuatia aliyekuwa katibu wa chama hicho Dk. Bashiru kupata uteuzi kwennye taasisi nyengine.

Endapo Samia atachukua nafasi hiyo atakuwa mwenyekiti wa sita akitanguliwa na mwaka 1990, Mwalimu Julias Kambarage Nyerere alipong’atuka madarakani alimkabidhi uenyekiti wa CCM Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Juni 1996.

Mwinyi naye alipomaliza ngwe zake za uongozi alikabidhi nafasi hiyo kwa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa ambaye naye ilipofika Juni 2006, alimkabidhi Jakaya Mrisho Kikwete na Julai 23, 2016, Kikwete alikabidhi kijiti hicho kwa Dk. Magufuli ambaye Machi 17, 2021 amefariki dunia.