MOGADISHU, SOMALIA
SOMALIA imepokea dozi 200,000 za chanjo ya virusi vya corona ya Sinopharm zilizotolewa na China ili kuisaidia kupambana na janga la virusi hivyo katika taifa hilo la pembe ya Afrika.
Waziri wa Afya na Huduma za Jamii wa Somalia, Fawziya Abikar Nur aliishukuru China kwa msaada huo wakati nchi hiyo ikipambana na janga la corona na kuongeza kuwa, watu 300,000 watafaidika na chanjo hiyo.
Nur alisema kuwa chanjo hiyo itasambazwa katika mikoa yote nchini Somalia na kwamba itaanza kutolewa kwa makundi yaliyohatarini kabla ya wananchi wa kawaida.
Balozi wa China nchini Somalia, Qin Jian alisema kuwa China itaendelea kuiunga mkono Somalia katika ujenzi wa amani, ukarabati, maendeleo na uboreshaji wa maisha ya watu nchini Somalia.
Jumla ya watu 12,406 wamethibitishwa kupatwa na maambukizi ya virusi vya corona ikiwa ni pamoja na vifo 618, kulingana na takwimu kutoka wizara ya afya nchini humo.
Wakati huo huo, taarifa kutoka nchini Somalia zinaeleza kuwa mashambulizi mawili yaliyofanywa katika maeneo tofauti nchini humo yameua zaidi ya watu saba na wengine zaidi ya wanane kujeruhiwa.
Mashambulizi hayo yalipangwa kwenye magari yaliyotegwa mabomu ambapo shambulizi la kwanza lilitokea katika mji wa Baidoa ambapo watu sita wameuawa na wengine saba kujeruhiwa.
Polisi katika mji huo walisema kuwa mtu aliyejitoa muhanga alijiripua katika gari aliyokuwa ameitega katibu na mkahawa, ambapo shabaha ya shambulizi hilo lilikuwa dhidi ya gavana ambaye alikuwa kwenye mkahawa huo akipata chai.