NA KHAMISUU ABDALLAH
DEREVA aliyedaiwa kusababisha msongamano barabarani, amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Farid Mohammed Mahmoud (25) mkaazi wa Amani wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Suleiman Jecha Zidi na kusomewa shitaka linalomkabili na Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Vuai Ali Vuai.
Ilidaiwa kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kuweka gari sehemu hatarishi, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Alidaiwa kuwa, Machi 10 mwaka huu saa 2:15 asubuhi huko Mwanakwerekwe kwenye mzunguko wa barabara, akiwa dereva wa gari yenye nambari za usajili Z 756 AG inayokwenda njia namba 516.
Akitokea Nyerere skuli kuelekea Mwanakwerekwe Polisi, alidaiwa kupatikana akiwa amesimamisha gari hiyo katikati ya barabara na kusababisha msongamano kwa watumiaji wengine wa barabara hiyo, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikubali na kuiomba mahakama impungunguzie adhabu kwa kudai kuwa ndio kosa lake la mwanzo, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa hauna kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshitakiwa huyo mahakamani hapo, hivyo adhabu itolewe kwa mujibu wa shitaka alilopatikana nalo.
Hakimu Suleiman, alimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 20,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki mbili.
Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda jela kwa muda huo.