NA HAFSA GOLO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, jana amejumuika na wananchi kuzuru kaburi na kumuombea dua eliekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Marehemu  Bregedia Jeneral Ramadhan Haji Faki.

Hafla hiyo imefanyika katika kijiji cha Mkwajuni, mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni muendelezo wa wiki ya kuwakumbuka  ya kuwaenzi viongozi wakuu wa kitaifa itakayofikia kilele chake Aprili 7, mwaka huu.

Alisema, serikali imeweka utaratibu maalumu wa kisheria  wa kuenzi, kuthamini  na kukumbuka fikra na mchango wa viongozi wa kitaifa waliotua katika kuijenga  Zanzibar na Tanzania kimaendeleo.

Dk.Khalid alisema, kupitia sheria namba 5 ya mwaka 2019, imeweka wiki ya mashujaa ambapo wananchi na viongozi hutumia siku za wiki hiyo ianyoanzia aprili 1 hadi 6 mwezi wa Aprili ya kila mwaka kuwa ni siku za maombolezo kwa viongozi wa kitaifa.

“Siku hizo zinakwenda sambamba na tarehe 7 April ambayo ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha Marehemu mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi ambae alifariki siku kama hiyo mwaka 1972,” aliongeza Dk. Khalid .

Katika hatua nyengine Dk.Khalid aliwahimiza wananchi kuendeleza kuenzi hekima na busara za viongozi hao sambamba na kuimarisha umoja na mashirikiano miongoni mwa jamii.

Mapema Kadhi wa Wilaya ya kaskazini ‘A’, Shehe Ali Zubeir, wakati akiongoza dua alisema serikali imefanya jambo jema la kuendelea kuwaombea dua viongozi hao kwani kufanya hivyo kunaongeza malipo mema kwao na wanaowaombea.

Nao wanafamilia waliishukuru serikali pamoja na kumtakia kheri Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ili aendelee kuiongoza Zanzibar kwa mafanikio makubwa.

Mbali na Dk. Khalid, katika hafla hiyo, viongozi mbali mbali serikali, vyama vya siasa na wanafamilia walihudhuria wakiongozwa na mkuu wa mkoa wa kaskazini unguja, ayoub mohammed Mahmoud na mkuu wa wilaya ya kaskazini ‘A; sadifa na vyama vyengine vya kisiasa.