NA MARYAM HASSAN

OFISI ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), imempandisha katika mahakama ya mkoa Mwera, mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 17 akituhumiwa kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 16.

Akiwa mahakamani hapo, mtoto huyo (Jina tunalihifadhi), alisomewa shitaka lake na Wakili wa serikali kutoka Ofisi hiyo ya DPP Sara Omar Hafidh, chini ya Hakimu dhamana Khamis Ali Simai.

Wakili huyo alidai kwa kuiambia mahakama kuwa, mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Januari 27 mwaka huu baina ya saa 2:00 na saa 5:45 za usiku, huko Pete wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa huyo, alidaiwa kumuingilia mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 16 ambae hajaolewa, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Baada ya kusomewa kosa hilo, mshitakiwa alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana, ombi ambalo lilikubaliwa kutokana na umri wake.

Upande wa mashitaka umesema hauna pingamizi juu ya kupewa dhamana kwa mshitakiwa huyo, lakini uliiomba mahakama kutoa masharti madhubuti juu yake.

Hakimu Khamis, alimtaka mshitakiwa huyo kusaini bondi ya shilingi 500,000 pamoja na kudhaminiwa na wadhamini wawili, ambao watamdhamini kwa maandishi kwa kiwango hicho hicho cha fedha pamoja na kuwasilisha mahakamani kopi ya kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi na barua za Sheha wa Shehia wanazoishi.

Alisema endapo mshitakiwa huyo atatimiza masharti hayo, atakuwa nje kwa dhamana hadi Aprili 14 mwaka huu kesi yake itapoanza kusikilizwa ushahidi.

Pia aliutaka upande wa mshitaka kwamba siku hiyo awepo Ofisa Ustawi wa Jamii, kama taratibu za sheria zinavyoelekeza kwa mshitakiwa aliyekuwa chini ya umri wa miaka 18.