WAISLAMU wote duniani katika siku chache zijazo watampokea mgeni

mtukufu wa Ramadhan na ujumbe wa heshima; nyoyo zinajifakharisha naye kwenye ujio wake na nafsi zinasubiria kuwasili kwake.

Kila mmoja wao anatarajia kufika huyu mgeni na kupata kheri na Baraka

zilizomo ndani yake.

Kwa hakika huu ni mwezi wa Ramadhaan uliobarikiwa, mwezi wa kheri na baraka, mwezi wa utii na kujikurubisha, mwezi wa Swawm na Qiyaam (kuswali usiku), kusoma Qur- an.

Ni mwezi wa kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kuomba

maghfira na kuomba du‟aa na kuomba kuokoka.

Aidha Mwezi mtukufu wa Ramadhani ndio msimu wa pekee ya ibada na kujikurubisha na Mwenyezi Mungu (S.W.), hivyo, mwislamu anatakiwa kujiandaa vizuri kimwili na kiroho kwa kutumia fursa hii katika ibada na kuizoesha nafsi kwa ibada na mema katika mwezi huu na baada ya kumalizika kwake.

Ramadhani ni fursa kubwa kwa waislamu wote duniani kurudi kwa Mola wao na kutafuta radhi na thwabu kutoka kwake. Kwa hiyo, msimu huu muhimu wa ibada na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu (S.W.) unahitaji maandalizi makubwa kiroho na kimwili, ambapo mwezi huu ni mfano wa soko la heri ambalo mwislamu anatakiwa kulitumia vizuri kwa ajili ya manufaa yake duniani na Akhera.

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi mtukufu. Katika mwezi huu milango ya Pepo inafunguliwa na milango ya Moto inafungwa.

Ni mwezi ulio bora kuliko miezi mingine. Katika mwezi huo, Mwenyezi Mungu Amewaneemesha waja Wake kwa kuwafungulia mlango wa matarajio kwa kuachwa huru na Moto.

 Mwenyezi Mungu, kila usiku miongoni mwa masiku ya Ramadhani, ana waachwa huru wajawake na Moto. Basi yapasa kwa Waumini wajitayarishe nayo na kujianda kupokeya kwa amali njema,wala sio kupokeya kwa masiya.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu (S.W.) Ameuelezea mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi bora kuliko miezi yote kwa kuwa Qurani imeteremka ndani ya mwezi huu unao usiku ulio bora zaidi kuliko miezi elfu moja nao ni usiku wa Al-Qadr.

Kwa mujibu wa Qurani Tukufu Mwenyezi Mungu Amebainisha kuwa Qurani imeteremka katika mwezi huu: {Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo waziza uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu na afunge.

Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru} [Al-Baqara: 185].

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, mwezi mtukufu wa Ramadhani umetukabili inatupasa tuupokee kwa kumcha Mwenyezi Mungu na kufanya twaa na ibada kwa wingi na kukaa mbali na maovu kama tunavyo jua ya kuwa malipo ya amali njema huongezeka na vile vile malipo ya amali mbaya.

Na mwezi huu mtukufu mwanzo ni kumi la rehma na kumi la maghfira na mwisho ni kuachwa huru na moto. Kufunga mchana ni wajibu na kusimama kwa ibada usiku ni sunna yenye kukamilisha faradhi.

Ukifunga kwa imani na kutarajia malipo utasamehewa madhambi yaliyotanguliia. Ukifanya ‘umra ni kama uliye hijji. Milango ya pepo hufunguliwa na ya moto hufungwa.

Na saumu ni ibada ya pekee ambayo Mola amejihusishia mwenyewe kama alivyosema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika hadithi ya Bukhari aliyoipokea kutoka kwa Abu Huraira kuwa Mwenyezi Mungu amesema [Amali zote za binaadamu ni zake ila saumu.

Hakika ya saumu ni yangu na ni Mimi ndiye nitakaye ilipa na saumu ni kinga, ikiwa ni siku ya mmoja wenu kufunga basi asifanye machafu, wala asiseme maovu, basi atakapo tukanwa na yoyote au akataka kupigana naye basi amwambie mimi nimefunga. Naapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi mwake harufu ya kinywa cha mmoja wenu ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski, na mwenye kufunga ana furaha mbili, moja huipata akifungua saumu, na ya pili ni wakati akikutana na Mola wake].

Enyi ndugu Waislamu, tujipinde katika mwezi wa Ramadhani kwani tusipo fanya hivyo tutakuwa mbali na rehma za Allah (Subhaanahu wa Taala) na kama tulivyobainisha ya kuwa twaewza tukafunga njaa iwapo hatutaepukana na makatazo ya Allah katika hali ya kufunga.

 Mwislamu anatakiwa kutumia fursa ya kupata maghufira na radhi ya Mwenyezi Mungu katika mwezi huu wa Ramadhani kwa kuwajibika mema na kuepukana na maovu, pia miongoni mwa mambo yanayotakiwa wakati wa kujiandaa kwa kupokea mwezi wa Ramadhani kurekebisha hali ya mahusiano ya mtu na Mola wake, jamaa zake, jamii yake na dunia kwa jula kwa kuwa mwezi huu unahitaji mtu mwenye moyo safi na nia njema aingie akiwa katika hali nzuri kitabia, kiimani na kisaikolojia.

Mtume (S.A.W.) na Maswahaba zake (R.A.) walikuwa wanajiandaa vizuri kwa ajili ya kupokea mwezi huu wakiwa na furaha na shauku ya kujikurubisha na Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza ibada zilizofaradhishwa na vinginevyo katika amali mema na matendo mazuri.

Namuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atufikishe sote kwenye mwezi waja Wake wenye taqwa na vipenzi Vyake waliokurubishwa ambao hawana hofu wala hawahuzuniki wa Ramadhaan na atusaidie juu ya kufunga na kusimama, na atengeneze mambo yetu, na aunganishe nyoyo zetu, na Atuongoze njia zilizo sawa, na atutoe kwenye kiza na kutuingiza kwenye nuru na atufanye miongoni mwa wajawema.

Imeandaliwa na Sheikh; Yasser Mohammed Fahmy

Mjumbe wa Kituo cha Kiislamu cha Misri

Dar es Salaam, Tanzania