NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ameuagiza uongozi wa mkoa Mjini Magharibi kurejesha mnada wa bidhaa katika soko la Mombasa (Shimoni) uliosimamishwa  kwa mwaka mmoja sasa.

Alitoa agizo hilo jana akiwa katika siku ya pili ya ziara yake katika mkoa huo alipotembelea maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Magharibi ‘B’, kwa lengo la kuangalia maendeleo na changamoto zilizomo katika wilaya za Unguja na Pemba.

Hemed alitoa muda hadi leo asubuhi mnada huo uliopo katika soko la Jumbi uwe umerejea katika soko la Mombasa ili kuwapa fursa wananchi na wafanyabiashara  unafuu ikiwa ni pamoja na kupata riziki zao za halali.

Alifahamisha kwamba si vyema wananchi wakalazimishwa kufuata bidhaa muhimu za vyakula katika masafa marefu  wakati uwezo wa kufuata huduma hizo katika masoko ya karibu unawezekana endapo kutawekwa utaratibu mzuri.

Aidha aliwataka wafanyabiashara kuendelea kufuata sheria na taratibu zilizowekwa  kwa vile serikali muda wote inawapenda wananchi wake  ambao nao kwa upande wao wana wajibu wa kuongeza ushirikiano wao kwa serikali.

Kuhusu milango ya biashara, Hemed alionya tabia ya mfanyabiashara kukodisha wenzao baada ya wao kupangishwa jambo linaloikosesha mapato serikali na kuutaka uongozi wa baraza la Manispaa Magharibi ‘B’ kuwajibika kwa kusimamia vyema upangisha wa milango na maduka katika soko hilo.

Aliwaeleza wafanyabiashara wa masoko ya Mombasa, Mwanakwerekwe na Jumbi kuwa serikali kuu kupitia Mabaraza ya Manispaa inaangalia mbinu muwafaka ya kujenga soko kubwa na la kisasa katika eneo la Wilaya ya Magharibi ‘B’ kwa lengo la kuwaondoshea msongamano wafanyabiashara wa Masoko hayo.

Akizungumzia changamoto ya mafuriko ya Mvua za Masika zinazoathiri maeneo ya makaazi, Hemed alisema Wahandisi na Washauri Elekezi  wanaosimamia miradi ya ujenzi wa barabara kujiepusha kufanya kazi kwa kuripua badala yake wazingatie mikataba ili kuondoa madhara.

Katika ziara hiyo, Hemed pia alitembelea bwawa la Jiangamizini kwa agizo la Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, linalojaa maji ya mvua hasa wakati wa msimu wa masika, alisema serikali itaunda kamati maalum kufanya utafiti utakaobaini chanzo cha ongezeko la maji katika bwawa hilo.

Alisema Kamati hiyo itakayoundwa na kutoa ripoti yake ndani ya kipindi kifupi kijacho itahusisha wataalamu wa kamisheni ya kukabiliana na maafa, mamlaka ya mazingira, ardhi na baadhi ya watu wanaoifahamu historia na mwenendo halisi wa bwawa hilo.

Mapema akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za serikali katika wilaya ya Magharibi ‘B’ katika ukumbi wa manispaa ya Magharibi ‘B’, Mkuu wa wilaya hiyo Hamida Khamis Mussa, alisema vitendo vya udhalilishaji vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku wilayani humo.

Alisema ongezeko hilo linatokana na kasi ya jamii kujitokeza kuripoti matukio ya vitendo hivyo ambapo matukio 150 yameshafikishwa katika mamlaka husika kwa hatua za kisheria.

Akigusia migogoro ya ardhi, Hamida alibainisha kwamba uuzaji wa viwanja kiholela kwa eka zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kilimo ambapo malalamiko 105  yameripotiwa na hadi sasa 67 yamepatiwa ufumbuzi wakati 38 ikiendelea kutafutiwa suluhu.

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitembelea jengo jipya la Mamlaka ya Chakula na Dawa linaloendelea kujengwa, kukagua shughuli mbali mbali za baraza la vijana wilayani humo pamoja na machinjio ya wanyama ya Kisakasaka.