NA NASRA MANZI

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah amesema umefika wakati kwa vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS), kutafuta wataalamu watakaosaidia kuwapatia maarifa ya uwekezaji wenye tija.

Hemed alisema hayo jana Magomeni mjini Zanzibar kwenye hafla ya kuzindua jengo la Elimu SACCOS lililopo Magomeni Jitini, ambapo hotuba yake ilisomwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini\Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa aliyemuwakilisha kwenye hafla hiyo.

Akizungumza na wanachama wa mkutano mkuu wa Elimu SACCOS wa 19 huko katika ukumbi wa Judo uliopo Amani, Hemed alisema baadhi ya vikundi vya akiba vina fedha zinazokidhi kufanya uwekezaji, hivyo ni vyema wakatafuta wataalamu kupata ushauri juu ya mradi mzuri wa uwekezaji.

Alisema fedha za SACCOS zinapowekezwa zitasaidia uwezo wa kifedha wa chama, kukuza uchumi wa nchi sambamba na kutoa ajira kwa wananchi.

Hemed aliwataka wanaushirika hao kuwa wabunifu, hali ambayo itawafanya kutoogopa changamoto na badala yake kuwa na fursa zitakazokuza maendeleo ya vikundi hivyo.

Alifahamisha kuwa mafanikio waliyoyapata wanaushirika hao sio tu yatatoa changamoto kwa SACCOS nyengine ambazo zinasuasua, lakini yanatoa ujumbe kwa serikali kuziwekea mazingira mazuri SACCOS zilizopo nchini hasa ikizingatiwa kuwa zina msaada mkubwa kwa jamii.

Aliwashauri kuongeza nguvu katika kutekeleza mipango yao na kuwapongeza kwa kujenga jengo kubwa ambalo watalitumia kama kitega uchumi kitakachoongeza mapato ya ushirika huo.

“Jengo lenu ni la kisasa ambalo limebadilisha haiba ya Magomeni jitini, litumieni kwa ajili ya kuongeza mapato na jitangazeni ili muongeze idadi ya wanachama”, alisema.

Alieleza kuwa amefarajika kuona ushirika umetoa ajira kwa vijana 18, hivyo ni vyema taasisi nyengine nchini kuiga mfano huo ambao unasaidia tatizo la ajira kwa vijana waliopo nchini.

Kwa upande wake Mrajis wa vyama vya ushirika, Khamis Daud Simba alisema sekta ya ushirika ina muelekeo mkubwa kwa mujibu wa sheria kwani inasaidia kuondosha changamoto za wanachama kwa kujiinua kiuchumi.

Akisoma risala kwa niaba ya wanachama wenzake mmoja wa viongozi wa SACCOS hiyo, Maneno Ibrahim alisema ushirika huo umepata mafanikio kipindi cha mwaka 2019 hadi 2020 ikiwemo kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa wanachama na wasio wanachama.

Alisema wamenunua boma la nyumba eneo la Magomeni na kujenga jengo la roshani kwa dhamira ya uwekezaji wa maduka, ukumbi, ofisi na ghala la kuhifadhia bidhaa.

Mbali na mafanikio hayo wanaushirika hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuondoshwa kwa utaratibu ambao wajasiriamali na vikundi vya ushirika kupatiwa fursa za safari za kujifunza katika nchi mbali mbali.

Alieleza changamoto nyengine kupitiwa upya sheria na kanuni ya ushirika ili kukidhi haja ya vikundi na vyama vya ushirika ambapo sheria iliyopo imekuwa ni kikwazo.

Ushirika huo wa Elimu SACCOS una jumla ya wanachama 1,785 wakiwemo wanaume 689 na wanawake 196.