AKIWA katika Kampeni za kugombea urais wa Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana, Dk. Hussein Ali Mwinyi, miongoni mwa ahadi alizoziweka ni pamoja na kupambana na ufisadi, rushwa, kutowajibika na upotevu wa fedha za umma.
Kama hivyo ndivyo kile ambacho wananchi tunakitarajia ndicho tunachokiona kwa sasa ambapo tayari Dk, Hussein ameanza kuchukua hatua stahiki kwa wale wanaokwenda kinyume na ahadi alizozitoa.
Hapo jana tumeshuhudia Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi akitengua uteuzi wa Makamanda watatu wa Idara Maalum za SMZ kufuatia kuwepo kwa wafanyakazi hewa na kusababisha upotevu wa fedha nyingi za Serikali.
Waliotenguliwa ni Kamanda wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar Ali Abdallah Ali, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kanali Ali Mtumweni Hamad pamoja na Mkuu wa Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) Comodore Hassan Mussa Mzee.
Kwa mujibu wa taarifa ya Rais Dk. Hussein kufuatia kamati iliyoteuliwa kuchunguza ufisadi huo inaonesha kuwa fedha zilizotumika kwa upotevu ni kiasi cha shilingi bilioni 2,235,725,000.00 kutokana na fedha zilizokuwa zikitumika kwa wafanyakazi hewa.
Vile vile, Kamati ilibaini ulipaji wa posho katika vikosi hivyo ambapo wastani wa upotevu wa fedha zilizokuwa zikilipwa kwa ajili ya posho kwa mwezi wa Disemba ni jumla ya shilingi milioni 304,135,939.00 sawa na wastani wa shilingi bilioni1,824,815,634.00 kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Disemba.
Sambamba na hilo, lakini kamati haikuishia hapo na iliendelea kubaini kwamba kuna watumishi ambao walikuwa wameshastaafu lakini bado walikuwa wakiendelea kupokea mishahara ambapo kulikuwa na wastaafu 12 wa Idara Maalum za SMZ waliokuwa wakiendelea kulipwa mishahara baada ya kustaafu ambapo ni kinyume na utaratibu.
Katika mambo yote hayo kimepelekea Serikali kuingia hasara ya jumla ya shilingi milioni 44,610,280.00.
Kwa mfano kikosi cha JKU Kamati ilibaini jumla ya askari 771 walikatwa fedha za posho ya chakula bila ya kukaa Kambini na fedha zao kuingia mifukoni mwa watu wachache kiasi cha shilingi 539,700,000.00kwa kipindi cha miezi 10 kuanzia mwezi wa Machi 2020 hadi Disemba 2020.
Utenguzi huo tumeupokea kwa moyo mkunjufu kabisa hasa kwa kuwa waliotenguliwa ni wasimamizi wakuu wa taasisi hizo jambo ambalo walipaswa kulisimamia na kulichukua hatua stahiki kwa maslahi ya umma.
Upotevu wa fedha nyingi za umma haukubaliki si tu kwa serikalini lakini hata katika taasisi binasi jambo ambalo linawanyima haki wengine na kuwapa wachache kwa maslahi yao.
Pamoja na kutenguliwa kwa nafasi zao hizo, tunaiomba serikali iwachukulie hatua kali za kisheria kwa wale wote waliohusika kwa njia moja ama nyengine katika ubadhirifu huo mkubwa wa fedha za Serikali kwa maslahi yao binafsi.
Sambamba na hilo tungeishauri Serikali pia kuzibinafsisha mali za watu hao kwa kuwa chumo kubwa linatokana na fedha hizo kiasi kwamba waliwanyima fursa nyingi za kijamii wananchi waliowanyonge kama huduma za afya, maji safi na salama, nishati, elimu, miundombinu ya barabara na huduma ambazo fedha hizo zingesaidia kuhudumia baadhi ya mambo hayo.
Kwa miaka kadhaa wafanyakazi wengi wa vikosi vya SMZ walikuwa wakilalamika namna ya wakubwa wao wanavyoamua kukata mishahara na fedha nyengine kwa sababu zisizokuwa na msingi, hivyo uamuzi huo wa kutengua nafasi hizo ungelikwenda sambamba na hatua za kali za kisheria.
Mchezo uliochezwa na Idara ya vikosi vya SMZ unawezekana sana ukachezwa katika taasisi nyengine hivyo, tunaiomba serikali ikawa na jicho kubwa la kuziangalia taasisi nyengine jambo ambalo litaleta sura nzuri kwa wananchi na hata taifa kwa ujumla juu ya mapambano ya rushwa ubadhirifu na kutowajibika kwa watumishi wa umma na hasa viongozi wa taasisi kuyafumbia macho maovu kwa maslahi yao.
Tunakuamini Rais Dk. Hussein kwa hatua zako hizo na tunakuunga mkono lakini ili kuona hayo yanafanikiwa Sheria ichukuwe mkondo wake ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.