NAIROBI, KENYA

SHIRIKA la Fedha Duniani (IMF) limethibitisha kuwa limeikopesha nchi ya Kenya shilingi za nchi hiyo bilioni 255 ambazo ni sawa na dola bilioni 2.4, kwa ajili ya kusaidia kudhibiti deni la umma.

Katika taarifa ya shirika hilo la kimataifa iliyowekwa kwenye tovuti, IMF imesema Kenya ilikuwa ikikabiliwa na changamoto za kifedha kutokana na madeni iliyokuwa ikiyalipa.

Shirika hilo lilifahamisha kuwa Kenya imejikuta katika dimbwi la mzigo wa deni lililochangiwa na maambukizi ya virusi vya corona ambavyo pia vimeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa taifa hilo.

Taasisi hiyo ya kimataifa ya kifedha ilieleza kuwa changamoto nyengine za kifedha ambazo Kenya inakabiliwa nazo, ziliainishwa katika bajeti ya nchi hiyo ya mwaka 2020/2021.

IMF inasema ina matumaini kuwa uchumi wa Kenya utaimarika mara tu nchi hiyo itakapofanikiwa kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Kauli ya shirika hilo imekuja siku chache baada ya baadhi ya raia wa Kenya kuitaka taasisi hiyo kusita kuikopesha pesa serikali ya rais Uhuru Kenyatta, kwa madai kuwa imejaa ubadhirifu.