NA MADINA ISSA

CHUO cha Utawala wa Umma (IPA) kimezindua programu ya mashirikiano ya kitaaluma kati ya chuo hicho na chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha IPA, Tunguu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sheria, Katiba, Utumishi na Utawala Bora, Haroub Ali Suleiman, alisema kufunguliwa kwa ngazi hizo kutawawezesha wataalamu mbalimbali wa ngazi hizo kuja kusoma Zanzibar kupitia chuo cha IPA.

Alisema kuanzishwa kwa mafunzo hayo, pia itawapunguzia usumbufu wa wanafunzi wa Zanzibar kwenda kutafuta elimu sehemu za mbali na nchi yao sambamba na kuweza kuzalisha wataalamu wengi zaidi.

Hata hivyo, aliupongeza uongozi wa UDOM na IPA kwa jitihada zao walizozifikia hadi kukamilika kwa mchakato huo ambapo kwa sasa wamewawezesha wananchi kusoma katika Cho hicho.

“Hakika mchakato huu umeanzia mbali sana na viongozi waliopita walilianza na viongozi waliokuwepo nao wamefanikisha hivyo sina budi kuwapongeza kwa kufanikisha suala hili” alisema.

Naye, Mkurugenzi wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA), Dk. Shaaban Mwinyichum Suleiman, alisema, mafunzo hayo ni sehemu ya makubaliano kati yao na UDOM ambayo yalikuwa mwaka mmoja uliopita.

Aidha alisema mbali na hayo, vyuo hivyo vimekubaliana kushirikiana katika utoaji wa mafunzo mafupi pamoja na kushirikiana katika tafiti mbalimbali.

Aidha alisema kuwa katika mafunzo hayo jumla ya watumishi 63 wamefanikiwa kupata nafasi ya kujiunga katika ngazi hizo katika fani mbalimbali ikiwemo uhusiano wa kimataifa, uhasibu na fedha, uongozi wa biashara, utawala, sayansi ya siasa, Uchumi, elimu na Sheria.

Hata hivyo, alifahamisha kuwa kati ya watumishi hao ni watumishi 44 kutoka IPA ambao wanaofanya shahada ya uzamili jumla yake ni 15 wanawake watano na wanaume 10 na shahada ya Uzamivu 29 kati ya hao wanawake 7 wanaume ni 22.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Chuo cha UDOM, Profesa Faustine Karran Bee, alisema kuwa imani ya chuo hicho ni kuona wanafunzi hao wanamaliza kwa muda uliopangwa na hawatopenda kuona watumishi hao wanachelewa kumaliza masomo na waendelee kutimiza wajibu wao wakati wote wa masomo.

Hata hivyo, alisema kuwa wajibu wao ni kuhakikisha walimu wanawasimamia katika masomo na kuhakikisha wanamaliza muda uliopangwa na wajitahidi kuhudhuria masomoni.

Aidha alisema kuwa chuo hicho kimekuwa na mahusiano na vyuo mbalimbali duniani ambapo mashirikiano huongeza tija sambamba na kupata mafanikio yanayoweza kufikiwa kwa pamoja.

Mapema, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha UDOM, Gaudentia Mugosi Kabaka na Mwenyekiti Chuo cha IPA, Fatma Said Ali, walisema kuzinduliwa kwa programu hiyo imedhihirisha kuwepo kwa ushirikiano wa vyuo hivyo kwa lengo la kuwapata watumishi waliokuwa na elimu zaidi.