NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo amesema serikali za Tanzania zina nia ya kuzimaliza changamoto zote zinazoukali muungano.

Jafo alieleza hayo alipokuwa akizungumza na gazeti hili kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika jengo la CCM lililopo Kisiwandui mjini Zanzibar, pembeni ya   kumbukumbu ya miaka 49 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, mzee Abeid Amani Karume.

Waziri huyo aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa serikali itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto za muungano ili kila upande uweze kwenda sawa.

Alisema anafahamu miongoni mwa changamoto kubwa ya kero za muungano ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi zaidi ni suala la kifedha na kodi, ambalo nalo alisema litapatiwa ufumbuzi. 

“Nimeingia juzi tu katika wizara hii, lakini nikiwa waziri kwenye maeneo mbalimbali ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haya mambo nayafahamu kwa kina na mengine tutayaibua ili tuweze kuyafanyia kazi,” alisema.

Aidha alisema malengo yake ni kuona maagizo aliyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika kushughulikia kero hizo anayatimiza kwa ufanisi.

Alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alikuwa katika wizara hiyo ya muungano kwa zaidi ya miaka 10, hivyo anajua kuna mambo lazima yanatakiwa kufanyiwa kazi.

“Kama nilivyofanya kazi takriban miaka mitano katika ofisi iliyokuwa na changamoto kubwa ya tawala za mikoa na serikali za mitaa, imani yangu kwamba yale yote aliyoniagiza rais katika wizara hii aliyonipa sasa nitayafanyia kazi na jukumu langu kuhakikisha kero zote tunaziondosha kwa upande wa bara na Zanzibar,” alisema.

Hata hivyo, waziri Jafo alibainisha kwamba kuzifanyia kazi changamoto za muungano na kuzitatua ni kuendelea na kudumisha Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar uliokuwa imara miaka yote.

Aliwaomba wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuimarisha muungano wao huku akiahidi kwamba changamoto ambazo zimekuwa ni donda ndugu dawa yake ni kuzipatia ufumbuzi.

Aliwasisitiza viongozi kufanya kazi kwa weledi, hekma, busara na kujituma kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu mbele ili waweze kutenda haki kwa watanzania.

“Kazi ni ibada kwangu kuhakikisha kwamba mambo ambayo ni changamoto kubwa tukiweza kuyatatua basi muungano wetu utazidi kuimarishwa,” alibainisha.

Aliahidi kwamba mambo ambayo yanaonekana ni changamoto kubwa yakiweza kutatuliwa basi maeneo yao, mahusiano yao na muungano wao utaendelea kuzidi kuimairika.

Aliahidi kufanya kazi kwa ueledi, hekma na busara ili kuona watanzania wanapata furaha ya muungano wao wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Jemedari Mzee Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wao.