NA MWAJUMA JUMA
UONGOZI wa klabu ya soka ya Jang’ombe Boys umesema kuwa kauli mbiu ya ‘Boys Tunatengeneza jambo letu’ haikuwa na maana ya kushinda kila mchezo watakaocheza.
Akiitolea ufafanuzi kauli mbiu hiyo Katibu wa klabu hiyo Alawi Haidar Foum hivi karibuni alipozungumza na waandishi wa habari huko katika ukumbi wa VIP Amaan.
Alisema watu wengi wameitafsiri vibaya kauli mbiu hiyo lakini kwa vile wanajua wanachokifanya, chochote ambacho hutokea katika mchezo huchukulia ni kawaida.
Alifahamisha kwamba boys wana dhamira ya kufanya mambo mengi katika kuijenga timu yao na kila mmoja anajua kwamba wanatengeneza jambo lao.
“Wengi walidhania kwamba kauli ya Boys tunatengeneza jambo letu walifikiria tunaposhuka uwanjani tutaifunga timu mabao tisa au 12 sio hivyo, bali ni vitu tofauti na malengo ya uongozi”, alisema.
Hata hivyo alisema bado hawajafeli malengo yao na wanaendelea kupiga hatua kila siku, kwani wamejiwekea malengo baada ya miaka minne kushiriki mashidano ya kimataifa.
Hivyo alisema wakiwa na malengo hayo ni dhahiri kwamba bado kuna miaka mitatu ya kujiandaa ili kufikia ligi kuu ili kufikisha hatua hiyo.
Timu ya Jang’ombe Boys inashiriki ligi daraja la kwanza Kanda ya Unguja ambapo hadi ligi hiyo inasimama ipo nafasi tisa katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 18.
Ligi hiyo inashirikisha timu 12 inaongozwa na Taifa ya Jang’ombe yenye pointi 34, ikifuatiwa na Uhamiaji ambao wana pointi 31 na nafasi ya tatu inashikiliwa na Mchangani FC wenye pointi 30.