Dk. Mwinyi aongoza visomo, dua

NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi jana amewaongoza wananchi, viongozi, vyama na serikali katika dua na kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar hayati Abeid Amani Karume.

Dua hiyo ilifanyika katika Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui ambapo viongozi wa dini ya kiislam, kikristo na wahindu walimuombea dua kiongozi huyo ikiwa ni miaka 49 toka alipofariki mwaka 1972.

Mbali ya viongozi hao wa kidini, viongozi wengine waliohudhuria katika dua hiyo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Sharif, Marais wastaafu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akitoa nasaha katika dua hiyo, Katibu wa Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Mfaume, alisema marehemu Mzee Abeid Amani Karume ataendelea kukumbukwa kutokana na kutandika misingi imara ya waafrika kujitawala wenyewe, kuimarisha umoja, mshikamano na kupendana.

Akinukuu msemo wa Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, “kuwa maisha ya mwanaadamu ni hadithi hapa ulimwenguni”, Khalid alisema ipo haja ya kila mtanzania kuwa hadithi nzuri kwa watakaosimuliwa.

“Mzee Karume alikuwa hadithi nzuri na ndio maana tunaendelea kumkumbuka jemedari wetu kwa mambo mazuri aliyotuachia,” alisema Mfaume.

Baadhi ya viongozi na wananchi waliohudhuria dua hiyo, walimzungumzia mzee Karume, kuwa alithubutu kuwatoa Wazanzibari katika utumwa wa kibeberu na kuwaweka huru katika nchi yao na kwamba ataendelea kukumbukwa kwa mengi aliyoyafanya kwa wananchi wa Zanzibar.

Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Catherine Peter Nao, alisema mzee karume anakumbukwa kwa mambo matatu ya msingi ikiwemo kutoa heka tatu kwa wananchi ili waweze kulima kwa ajili ya kujipatia riziki.

“Jambo jengine atakaloendelea kukumbukwa kiongozi huyo ni kuifanya elimu bure ili kila mtoto apate haki ya kusoma bila ya malipo na kutoa matibabu bure na kujenga misingi ambayo haitoweza kusahaulika kwa vizazi vya sasa na vitakavyokuja,” alisema.

Naye waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, alisema siku hiyo ni muhimu kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kwani hayati Karume alikuwa ni kiongozi mwenye maono na matarajio ya kuwaona watanzania wanaishi kwa umoja, amani na mshikamano.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema Mzee Karume ambae aliuawa na wapinga maendeleo, alikuwa ni kiongozi aliyewakomboa wananchi wa Zanzibar ambao katika uongozi wake aliweka alama ambayo haitofutika milele.

“Uongozi wake ni wa mfano na unafaa kuingwa na kila kiongozi katika taifa hili na nikitizama mwenendo, mtazamo na muelekeo wa serikali ya awamu ya nane unatupa matumaini makubwa kwamba unaakisi mwelekeo wa utekelezaji wa Mzee Abeid Amani Karume,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mkoa wa Magharibi, Zainab Ali Maulid, alisema,Marehemu Karume ana kila sababu ya kuenziwa kwani alisimamia mapinduzi ya ukombozi na kusimamia mapinduzi ya maendeleo kwa wananchi wake ambapo kila Rais anaendeleza mambo hayo.

Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema anapokumbukwa mzee Karume basi anakumbukwa mtu muhimu sana kwa Zanzibar kwani alikuwa ni kiongozi jasiri, jemedari hasa pale alipohakikisha kila mzanzibari anakuwa na uhuru wake.

Aidha alisema Wazanzibari na Watanzania wana kila sababu ya kumuombea kwani hayati Karume alikuwa na malengo yaliyoendana na matakwa na matarajio ya wazanzibari na kushuhudia maendeleo makubwa kutokana na viongozi waliomtangulia kuyafata maono na fikra zake.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na  Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohammed, alisema Zanzibar imekuwa ikiendeleza maono ya hayati Karume na kujivunia kuendeleza umoja, amani na mshikamano.

Aidha alisema ni imani kwamba yale yote aliyoyaacha yanaendelea kuendelezwa na viongozi wakuu wa serikali kuanzia awamu ya pili hadi awamu ya nane iliyokuwepo madarakani.

Alisema alama zote alizoziacha zinaendelezwa mpaka leo ikiwemo alama ya elimu bure ambayo inatolewa bila ya ubaguzi, matibabu bure, makaazi bora, kuwatunza wazee na watoto yatima.      

Akizungumzia kumbukizi hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Sadala (Mabodi) alisema licha ya miaka 49 kupita toka kifo cha mzee Karume kitokea, kimebakia kuwa elimu tosha kwa wananchi kuyaendeleza yale yote aliyoyaacha jemedari huyo.

Hivyo, aliwaomba wananchi kuendelea kudumisha Mapinduzi ambayo ndio historia kubwa katika nchi yao na kutunza hazina ya nchi yao ikiwemo wazee na hazina ya nchi ikiwemo maendeleo, watu na umoja wao katika kufanya kazi na kujituma ambayo ndio nguzo kuu aliyoiacha marehemu Karume.