BUJUMBURA, BURUNDI

JENERALI wa zamani wa jeshi la Burundi, Cyrille Ndayirukiye ambaye alikuwa anatumikia kifungo cha maisha jela kwa shutma za kujaribu kuuangusha utawala wa hayati rais Pierre Nkurunziza amefariki akiwa gerezani.

Ndayirukiye alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani Mei 13 mwaka 2015, aliaga dunia akiwa katika gereza la mkoa wa Gitega, katikati mwa Burundi, vyanzo vya habari nchini humo vimesema.

Kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni, Iwacu, Jenerali Ndayirukiye alifikwa na  mauti gafla baada ya kupatwa na kizunguzungua alipokuwa anaanika nguo zake alizozifua.

Aidha taarifa zinaeleza kuwa lisaidia na mfungwa mwenzake kwa kumuinua hata hivyo wakati anainuliwa sehemu ya mwili wake ulipooza na hakuamuka tena.

Maofisa wa serikali ya Burundi, wajatoa taarifa kuhusu kifo chake. Mtandao mwengine wa habari “SOS media Burundi, nao pia umethibitisha kifo cha Jenerali huyo.

Cyrille Ndayirukiye alikua miongoni mwa maofisa wa jeshi waliongoza jaribio la kutaka kumuondoa madarakani rais wa zamani wa Burundi Pierre Nkurunziza, Mei 13 Mei mwaka 2015, ambae wakati huo alikua jijini Dar es Salaam kushiriki mkutano wa kilele wa ma rais wa nchi wanachama wa jamuia ya Afrika mashariki.

Jaribio hilo lilizimwa na wanajeshi watiifu kwa Nkurunziza. Ndayirukiye na wenzake wa tatu walijisalimisha asubuhi ya Mei 14 mwaka 2015 na kuchukuliwa hatua za kisheria zilizosababisha kuishia kutumikia kifungo cha maisha gerezani.

Burundi iliingia katika mzozo wa kisiasa tangu Mei 2015. Mamia ya wafuasi wa upinzani walioshiriki maandamano ya kupinga muhula wa tatu wa rais wa wakati huo Pierre Nkurunziza, inadaiwa waliuawa, na maelfu ya wengine kufungwa jela, huku zaidi ya watu 400,000 wakikimbilia katika nchi jirani.