PALMA, MSUMBIJI
JESHI la Msumbiji limetangaza limeukomboa mji wa mwambao wa Palma uliopo kaskazini mwa nchi hiyo ambao ulikuwa chini ya wapiganaji wa itikadi kali wenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu.
Msemaji wa jeshi la Msumbiji kwenye eneo hilo, Chongo Vidigal alisema jeshi limechukua udhibiti wa mji wa Palma ambao umekimbiwa na watu tangu walipokimbia shambulizi la kigaidi lililotokea mwezi uliopita.
Mnamo Machi 24 kiasi wanamgambo 100 walivamia na kuushambulia mji wa Palma wenye utajiri mkubwa gesi asili na baadaye kundi la IS lilisema limeukamata mji huo na pia limewauwa wanajeshi 55 wa jeshi la Msumbiji.
Kwa zaidi ya miaka mitatu jimbo la Cabo Delgado lenye mji wa Palma limeshuhudia mashambulizi makali ya wapiganaji wa itikadi kali ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya raia na wengine kadhaa kuyakimbia makaazi yao.
Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa idadi kubwa ya waasi wameuawa kwa kupigwa risasi na vikosi vya Msumbiji katika operesheni ya kujaribu kuudhibiti mji wa Palma.
“Bado peresheni haijamalizika, lakini idadi kubwa ya magaidi wameuawa kwa katika operesni hiyo,” kamanda wa operesheni huko Palma, Chongo Vidigal, aliwaambia waandishi wa habari.
Maelfu ya wakaazi wa mji huo wameyakimbia makaazi yao kwa kuhofia usalama wao baada ya magaidi kuvamia mji huo na kusababisha maafa. Wakaazi hao wa Palma wamekimbilia mjini Pemba na wengi wao wanasema wanaogopa kurejea tena nyumbani.