NA MWANDISHI WETU

JUMUIYA ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA), imesema, itaendelea na kesi waliyofungua mahakamani dhidi ya Bodi ya Udhibiti Vileo Zanzibar mpaka hukumu itakapotolewa Juni 2 mwaka huu.

JUMAZA imefungua kesi namba 3 ya mwaka 2021 wakidai Bodi ya Udhibiti Vileo imevunja sheria 9 ya mwaka 2020 kwa madai ya kutoa vibali kwa kampuni za kuingiza vileo zaidi ya saba badala ya tatu kinyume na sheria na kifungu cha 33(1) cha sheria.

Akizungumza huko Makao Makuu ya Ofisi za JUMAZA, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Sheikh Ali Amour, alisema, kuna kiongozi mmoja wa JUMAZA ameitwa na kuombwa aiondoshe kesi mahakamani ili madai yao yamalizwe nje ya mahakama jambo ambalo hawapo tayari kulifanya.

Alisema JUMAZA imefungua kesi baada ya sekreterieti yake kujiridhisha umefanyika uvunjwaji na ukiukwaji wa sheria mpya ya vileo uliofanywa na Bodi ya Udhibiti wa Vileo baada ya sheria kupitishwa Baraza la Wawakilishi na kuanza kutumika baada ya kusainiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mei 11 Mwaka 2020.

“Hatujaona hoja zozote za msingi, hivyo kesi itaendelea mahakamani”, alisisitiza. Aliongeza kusema, “Kazi ya Bodi ya Vileo Zanzibar inatakiwa kusimamia sheria na siyo kuvunja sheria iliyopitishwa na chombo halali cha kikatiba cha kutunga sheria”.

Sheikh Ali alisema JUMAZA inaendeshwa kitaasisi na maamuzi yote hufanyika kupitia vikao vya uongozi ikiwemo sekeiterieti na bodi, hivyo haiwezi kufuta kesi kienyeji bila ya kupata ridhaa ya kupitia vikao vya pamoja.

“JUMAZA kabla ya kwenda kufungua kesi ilishauriana na wanasheria wake ikajiridhisha kuwa bodi ya vileo imevunja kifungu cha 33 (1) cha sheria ya vileo baada ya kutoa vibali kwa kampuni nane za uingizaji vileo Zanzibar badala ya tatu kinyume na sheria”.

“Kibali cha kuagiza kitatolewa kwa waagizaji wasiozidi watatu kwa kuzingatia vigezo kwa muingizaji lazima awe ni Mzanzibari, mlipa kodi, awe na ghala na gari ya kusambazia vinywaji”, alikinukuu kifungu cha 33(1) cha sheria mpya ya vileo namba 9 ya mwaka 2020.

Aidha, alisema, pia bodi ya vileo imevunja kifungu cha sheria cha 28(k) kinachosema leseni ya kuuza au kuhifadhi vileo ghalani itayotolewa kwa baa au ghala lazima kuwe na umbali wa mita 1,000 kutoka katika shughuli za huduma za kijamii, kama hospitali, skuli, nyumba za ibada au makaazi, lakini, imeshindwa kusimamia masharti ya sheria hiyo.

Kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa maandishi Mei 3 na 17 kabla ya hukumu kutolewa Juni 2 mwaka huu.