NEW DELHI, INDIA
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Afya Dunia (WHO) amezungumzia mgogoro wa maambukizi ya virusi vya corona nchini India na kusema kuwa, hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 nchini humo inaumiza sana.
Tedros Adhanom ambaye alikuwa akizungumza na waandishi habari ametahadharisha kuhusu wimbi kubwa la maambukizi ya corona ambalo halijawahi kushuhudia huko nyuma na vilevile idadi kubwa ya vifo vinavyosababishwa na maambukizi ya virusi hivyo nchini India na kusema kuwa, Shirika la Afya Duniani linatafuta njia ya haraka ya kusaidia juhudi za kukomesha mogoro huo.
Matamshi hayo ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO yametolewa huku India ikisumbuliwa na wimbi kubwa la maambukizi ya virusi vya corona na hospitali za nchi hiyo zikiwa zimejaa wajonjwa wa Covid-19.
Mkurugenzi huyo alisema WHO, linafanya kila linalowezekana katika kusambaza vifaa muhimu na nyenzo nyingine katika kuwanusuru raia.
Ripoti kutoka New Delhi zinaeleza kuwa, hadi kufikia saa mbili asubuhi jana, zaidi ya watu 2,600,000 walilazwa hospitalini au wanapatiwa matibabu na uangalizi wakiwa majumbani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mfumo wa afya na tiba wa India umeelemewa na mzigo wa idadi kubwa kupindukia ya wagonjwa huku idadi ya vitanda vilivyoko kwenye hospitali za nchi hiyo ikiwa haikidhi mahitaji ya wagonjwa wengi kupindukia waliopo wa maradhi ya Covid-19 yanayosababishwa na virusi vya corona.
Wakati huo huo hospitali nchini India zinakabiliwa na uhaba na ukosefu mkubwa wa mitungi ya oksijeni.
Zaidi ya watu milioni 17 wamepatwa na virusi vya corona nchini India.