KIGALI RWANDA
RAIS Paul Kagame wa Rwanda ameipongeza ripoti iliyotolwa na Ufaransa inayoainisha jukumu la nchi hiyo katika mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994.
Akizungumza mbele ya viongozi mashuhuri mjini Kigali, siku ya kwanza ya wiki ya kumbukumbu ya mauaji hayo, Kagame alisema ni jambo zuri kusonga mbele kwa kufahamu kile kilichotokea miaka 27 iliyopita.
Kagame alisisitiza tafsiri ya serikali yake ya matokeo ya uchunguzi wa tume ya Ufaransa kwamba rais wa Ufaransa wakati huo Francois Mitterand alifahamu mipango na utekelezwaji wa mauaji ya halaiki nchini humo.
Hata hivyo rais huyo aliendelea kuwaunga mkono wahutu waliofanya mauaji hayo kwa sababu aliamini yalikuwa muhimu kwa nafasi ya Ufaransa katika siasa za kikanda kwa wakati huo.
Hii ni mara ya kwanza Kagame kuizungumzia ripoti ya mauaji ya halaiki, ambapo inakisiwa watu takriban 800,000 waliuliwa na wauaji wa kihutu wakiwemo Watutsi na Wahutu waliojaribu kuwatetea, katika kipindi cha siku 100 za mauaji hayo.
Katika hatua nyengine Kagame alisema kwamba serikali na wananchi kwa ujumla hawatakubali kufumba macho wakati waliofanya mauaji hayo wakiendelea kubeza kutokea kwa mauaji hayo.
Katika hafla hiyo rais huyo alisema kuwa mauaji ya kimbari yamesababisha machungu zaidi kwa manusura hasa kuwaona baadhi ya wafanyaji wakipewa hifadhi katika nchi za kigeni bila ya kuchukuliwa hatua.