NA MADINA ISSA
WAKAAZI wa Shehia ya Charawe Wilaya ya Kati wameiomba serikali kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kuchukua juhudi za makusudi za kulitangaza na kuliimarisha eneo la pango la Charaweni ambalo limegundulikana miaka miwili nyuma.
Wakizungumza mara baadaa ya Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja, Rashid Hadidi Rashid, kufanya ziara ya kutembelea eneo la msitu wa Hifadhi Jozani, pamoja na kulikagua pango la Charaweni la Charawe na pango la Pange juu la Kitogani
Wananchi hao wamesema pango hilo la charaweni lenye vivutio mbali mbali vya kitalii wakiwemo ndege aina ya popo ambalo linasadikiwa kuwa lina miaka ya zaidi ya karne mbili sasa.
Alisema pango hilo wameshalitolea taarifa katika taasisi zinazohusika, lakini hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwaa katika kulifanya kuwa kivutio cha utalii.
“Tumeshalitolea taarifa sehemu husika ila wahusika hawajalifanyia chochote jambo ambalo linakosesha pia mapato ya serikali, kwani lingewekwa katika mapango pia lingeweza kuingiza fedha serikalini kwani watalii wangefika pamoja na wanannchi” walisema.
Aidha, wamefahamisha kuwa eneo hilo litaimarishwa na kuwa kivutio cha utalii na litawasaidia kwa kiasi kikubwa wakaazi wa kijiji hicho hususan vijana kuweza kupata ajira. na kuondokana na tatizo la uharibifu wa mazingira kwa kukata miti onyo, katika msitu wa hifadhi na maeneo mengine ya kijiji hicho.
Nae, Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja, Radhid Hadidi Rashid, aliwataka wananchi hao kuendelea kulitunza pamoja na kuhifadhi mazingira, ili kuliongezea haiba ya kuvutia.
Alisema wakati serikali inaendelea kuchukua juhudi za kukutana na waadau mbali mbali, ili kuona kwamba azma ya waananchi hao inafikiwa kwa lengo la kuleta maslahi ya taifa na waanakijiji hao kwa ujumla.
Alisema Mkoa wa Kusini Unguja ni miongoni mwa mikoa iliyobarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo mapango maarufu la Miza wa Miza la Kizimkazi, Kuumbi Jambiani Mfumbwi, na Majengo ya kihistoria Bihole Bungi na Mwinyi Mkuu.
Alisema hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa taasisi husika kuviimarisha na kuvitangaza vyanzo vipya viliomo ndani ya mkoa huo, ili kuiwezesha serikali kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii.