NA MADINA ISSA

ZAIDI ya chupa 560 za damu zimepatikana katika bonanza la uchagiaji damu katika wilaya ya Kaskazini ‘B’, kwa lengo la kupunguza vifo vinavyotokana na upungufu wa damu.

Akifungua bonanza la uchangiaji damu huko, Mahonda  uwanja wa mpira Misuka, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema bado mahitaji ya damu yanahitajika zaidi katika benki ya damu, ili kuweza kuokoa maisha ya mama wajawazito na watoto pamoja na majeruhi wengine wanaotokana na ajali.

Alisema ni vyema kwa wananchi kuwa na utaratibu wa kuchangia damu pindi inapohitajika hasa katika mabonanza yanayoweka katika mikoa, ili kukidhi mahitaji ya sasa na baadae.

Aidha alifahamisha kuwa kwa upande wa wilaya ya Kaskazini ‘A’ jumla ya chupa 401 za damu zilipatikana ambapo hadi kumalizika zoezi hilo katika mkoa huo jumla ya chupa 965 za damu zimepatikana.

Hivyo, aliwataka watendaji wa mkoa wa Kaskazini Unguja kuwajibika na kufanyakazi kwa uwadilifu ili kila mmoja kutimiza wajibu wake na mkoa huo kuweza kupiga hatua za maendeleo.

Meneja Benki ya damu, Bakari Hamadi Magarawa, alisema zoezi la uchangiaji damu litafanyika katika mikoa yote Unguja na Pemba, ikiwa ni mpango kazi wa mahitaji ya damu kwa kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Aidha alifahamisha kuwa malengo ya benki hiyo kwa sasa ni kukusanya chupa za damu 2000.

Kwa upande wao waliochangia damu, wamesema wameona umuhimu wa kuchangia damu kwa hiyari kwani uhitaji wa damu ni mkubwa kwa jamii na serikali na kuona vifo zinapingua kutokana na ukosefu wa damu.