NA JUMA RAMADHAN, OUT

KENYA ipo mbioni kumteua jaji mkuu mpya wa kwanza mwanamke. Na hii inafuatia hatua ya ya rais wa taifa hilo Uhuru Kenyatta kuliwasilisha jina la jaji Martha Koome bungeni.

Lengo hasa na madhumuni ya kufanya hivyo, ili apigwe msasa ana kura kupigwa iwapo ataidhinishwa kuichukua nafasi hiyo iliyowachwa wazi na David Maraga ambaye alistaafu.

Jaji huyo wa mahakama ya rufaa atakuwa jaji mkuu wa 15 wa Kenya, tangu nchi hiyo ijinyakulie uhuru iwapo bunge litaidhinisha uteuzi wake.

Mitandao mbali ya kijamii pamoja na vyombo vya habari vya kielektriniki kama vile ‘BBC’ vimekuwa vikisema kuwa, tume ya huduma kwa idara ya mahakama ilimtangaza Koome.

Mwanamama huyo, mwenye umri wa miaka 61, kama mshindi wa mahojiano kati ya watu wengine 10 waliotuma maombi ya kupewa kazi hiyo.

Bunge sasa litajadili uteuzi wake, katika kinachoonekana tu kama utaratibu lakini anatarajiwa kuidhinishwa na kuteuliwa rasmi na rais.

Koome atahudumu nafasi hiyo ya ujaji mkuu, kwa miaka tisa ijayo, ambayo itasheheni vipindi viwili vya uchaguzi na uwezekano wa kuandaliwa kwa kura ya maoni kuhusu katiba mpya.

Anakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinamngoja afisini ambazo watangulizi wake walijaribu kadri ya uwezo wao kuzishughulikia, lakini bila mafanikio waliotarajia.

Martha Koome ni mwanamke wa aina gani?

Jaji Martha Koome alizaliwa katika Kijiji cha Kithiu, katika kaunti ya Meru 1960. Baadaye alisomea shahada ya sheria katika Chuo kikuu cha Nairobi ambapo alifuzu 1986 na na kujiunga na chuo cha mafunzo ya Sheria nchini Kenya mwaka uliofuata.

Alianzisha Ofisi yake ya huduma za uanasheria 1988, na baadaye akajiunga na huduma ya mahakama 2003 na kuhudumu katika mahakama tofauti kote nchini.

Wakati ambapo pia alihudumu kama mwanachama wa chama cha wanasheria nchini Kenya LSK.

Mwanamke huyo shupavu, baadaye alijiunga na Chuo kikuu cha London, ambapo alisomea shahada ya uzamili kuhusu sheria ambapo alifuzu na kupata cheti cha Sheria ya Umma ya kimataifa 2010.

Mwaka 2011, alipandishwa cheo na kuwa Jaji wa mahakama ya rufaa, ingawa mwezi Septemba mwaka huohuo, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Muungano wa Mahakimu na Majaji nchini Kenya.

Jaji Koome, katika kipindi chake cha miongo mitatu amekuwa mtetezi wa haki za wanawake na ustawi wa watoto kwa ujumla.

Kuna wakati mmoja alihudumu kama Mwenyekiti wa baraza la kitaifa la Jopo Maalum, kuhusu usimamizi wa haki za watoto ambapo alisaidia katika kufanyia marekebisho sheria ya watoto.