NAIROB, KENYA
MZOZO kati ya Kenya na Uingereza umeendelea kutokota baada ya serikali ya taifa hilo la Afrika Mashariki kutangaza masharti mapya kwa abiria wanaotoka au kupitia Uingereza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara mambo ya nje ya Kenya, masharti hayo yataanza kutekelezwa rasmi kuanzia Aprili 9 mwaka.
Uamuzi huo uliochukuliwa na Kenya unaonekana kama ulipizaji kisasi, kufuatia hatua ya Uingereza kupiga marufuku abiria wote wa ndege waliopitia au kutoka nchini Kenya.
Aidha taarifa hiyo inaeleza kwamba abiria kutoka Uingereza ni sharti wawe na vyeti vya kuonyesha kuwa hawana virusi vya corona na kwamba wamepata chanjo ya ugonjwa huo.
Sharti jengine ililowekwa na Kenya ni kwa abiria hao kuagizwa kujitenga na watu wengine kwa siku saba baada ya kuwasili nchini kutoka nchini Uingereza.
Aidha ndege za mizigo hata hivyo, hazijaorodheshwa kwenye marufuku hiyo, ila marubani na wafanyakazi wake wengine ni sharti wawe na vyeti vinavyohitajika, vya kuonyesha hawana virusi na tayari wamepewa chanjo.
Wiki iliyopita Uingereza iliziongeza nchi za Kenya, Ufilipino na Bangladesh, kwenye orodha ya nchi ambazo, abiria wake hawataruhusiwa kuingia nchini humo.