NA MWANDISHI WETU
MUUNGANO wa Tanzania sasa umetimiza miaka 57 tokea kuasisiwa kwake mwaka 1964 chini ya marehemu Mwl. Julius Kambarage Nyerere na mzee Abeid Amani Karume.
Yapo mengi ya kujivunia chini ya muungano huu, kubwa la kupigiwa mfano ni kuendelea kuwepo amani na utulivu wa nchi na wananchi kwa ujumla kwa ajili ya maendeleo ya taifa lao.
Historia inatuonesha kwamba mara baada ya kuundwa serikali mpya ya Afro Shirazi ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ikiongozwa na Baraza la Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake Marehemu Mzee Karume, viongozi wa Tanganyika na wa Zanzibar walianza mazungumzo ya kuungana.
Lengo na msingi ilikuwa kurudisha kiserikali, udugu na umoja wa watu wa Zanzibar na Tanganyika kama ilivyokuwa kabla ya wakoloni hawajaigawa na kuitawala Afrika.
Nchi mbili huru, kama zilivyokuwa Zanzibar na Tanganyika zinapoungana, kuna njia mbili za kuziunganisha. Njia ya kwanza ni kuungana kwa yale wanayokubaliana, hata yakiwa ni machache, madamu nia ipo ni kutekeleza ile nia na halafu zikaendelea kutanzua matatizo yao na kujenga juu ya ile nia iliyokwisha kutekelezwa.
Njia ya pili ni kukaa na kutanzua matatizo kwa makubaliano mpaka kifikie kima cha makubaliano kiwezacho kuleta muungano. Zote hizi njia mbili si rahisi na kila moja ina matatizo yake yanayoweza kuchukuwa muda mrefu kutanzuliwa.
Tanganyika na Zanzibar zilichagua njia ya kwanza, siyo kwamba ndiyo iliyokuwa rahisi, bali kwa sababu nchi hizi mbili zilikubaliana kutekeleza nia yao ya kuungana na kutanzua matatizo yaliosalia ya muungano huku zimo katika muungano.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa watu uliofanywa na watu wenyewe chini ya uongozi wa Mwl. Julius Nyerere na Marehemu Mzee Karume, kwa manufaa ya watu wa Tanzania wenyewe.
Baada ya mazungumzo mafupi tarehe 22 Aprili mwaka 1964, Mwalimu Nyerere alifika Unguja ambako makubaliano ya kuungana yalifikiwa na siku nne baadaye yakathibitishwa huko Dar es Salaam katika kikao maalum cha haraka cha Bunge la Tanganyika lililoitihswa na Rais Nyerere Aprili 25,1964 kuthibitisha mkataba wa muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Wakati akilihutubia Bunge, Mwalimu Nyerere alielezea umuhimu wa kitendo hicho cha kuziunganisha nchi mbili jirani ambazo ziliwahi kuwa nchi mmoja kabla.
Matumaini ya Bara la Afrika kujenga umoja na bara hilo zima na kukuzwa kwa matumaini hayo kutokana na Muungano wa Zanzibar na Tangayika.
Mwalimu akilifahamisha Bunge maana ya Muungano na shabaha ya Umoja wa Afrika, alisema, “Ikiwa nchi ambazo ni marafiki na ni jirani na hasa zile ambazo zilipata kuwa moja bali zikagawanywa na wakoloni, ikiwa nchi hizo zitashindwa kuungana na kushindwa huko kunaweza kulata wasiwasi katika bara letu la Afrika na shauku yake ya umoja, bali ikiwa nchi hizo zinaweza kuungana, Muungano huo wawezakuwa thibitisho la vitendo kwamba matumaini ya bara letu si ya bure”.
Mwalimu alizidi kulifahamisha Bunge njia za pamoja za kufikia lengo la Muungano wa nchi za Afrika zinavyoweza kuungana na kuwa kitu kimoja. Baadaye alilidokeza Bunge uhusiano wa kidugu uliokuwepo baina ya Tanganyika na Zanzibar na jinsi nchi hizi mbili zilivyoshirikiana.
Bunge la Tanganyika liliuthibitisha mkataba wa Muungano kama viongozi wakuu wa nchi mbili hizo walivyokwisha kukubaliana na kukatibiana.
Kitendo cha Muungano kilikamilishwa na Rais Karume akifuatana na Mawaziri, Memba wa Baraza la Mapinduzi, Wakuu wa Chama na Serikali walipofika Dar es Salaam tarehe 26 Aprili 1964, kutia sahihi mkataba wa Muungano.
Ukurasa mpya wa historia ulifunguliwa na viongozi hao shupavu wenye kuenzi udugu na kuthamini umoja wa Afrika.
UCHAGUZI WA RAIS 1965
Mwaka 1965, ulikuwa ndio mwaka wa mwanzo kwa wananchi wa Tanzania kupiga kura kumchagua rais wa Tanzania baada ya Muungano wa 1964. Kila raia wa Tanzania aliyefikia umri wa miaka 21 alikuwa ana haki ya kuajindikisha katika kituo cha kupigia kura.
Uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Septemba ulitoa nafasi kwa wajumbe wengi zaidi kuingia katika Bunge.
Rais Nyerere tarehe 10 Septemba 1965, aliwachagua kwa mujibu wa katiba jumla ya wajumbe 47 kuingia katika bunge, miongoni mwao wakiwa wajumbe 23 wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na wajumbe wengine 14 wa Zanzibar ambao hawamo katika Baraza hilo, pamoja na wajumbe 10 wengine aliowachagua kwa kufuata kifungu cha 33 cha katiba. Katika hao 10, sita walikuwa kutoka Tanganyika na wanne kutoka Zanzibar.
HALI YA SASA YA MUUNGANO
Juhudi zinafanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kero za muungano ambapo kwa sasa zimebakia chache.
Ni juhudi ambazo zinatakiwa kupongezwa na kuungwa mkono kwa vile haikuwa kazi rahisi kufikia kiwango hicho cha ufumbuzi wa kero hizo huku wapinzani wakizitumia kujenga ajenda za kuhatarisha muungano.
Pamoja na kuwepo na changamoto mbali mbali, kamati ya pamoja ya kushughulikia kero na masuala ya muungano yenye wajumbe kutoka serikali zote mbili chini ya aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, abaye sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, iliendelea katika hatua za mwisho za kutatua kero zilizobakia kwa lengo la kuimarisha mfumo huo wa kiutawala.
Ufumbuzi wa kero 15 zilizokuwepo ni kielelezo tosha cha kuonesha dunia kwamba chini ya utawala wa serikali zinazotokana na Chama cha Mapinduzi, hakuna kisichowezekana katika utekelezaji wa mambo yanayogusa maisha ya wananchi wa pande zote mbili za muungano.