NA HAFSA GOLO
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar imetoa ruhusa ya kutumika kwa muda kituo cha daladala cha Michenzani (maarufu tobo la pili).
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Rahma Kassim Ali alieleza hayo jana wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.
Alisema daladala zote zitaruhusiwa kupakia na kushusha abiria kwa pande zote mbili katika eneo hilo.
Aidha Waziri Rahma alisema kwamba utekelezaji wa zoezi hilo utaanza rasmi leo huku akihimiza ushirikiano ili kuondosha vikwazo kwa dereva atakaekwenda kinyume na agizo hilo.
“Tumekusudia kuwapunguzia wananchi usumbufu wa usafiri”, alisema.
Alifahamisha kwamba hatua ya maamuzi hayo imekuja kwa mujibu wa uwezo aliopewa na kifungu cha 157(1) (A) cha sheria ya usafiri barabarani namba 7 ya mwaka 2003.
Alisema kifungu hicho kimempa uwezo wa kuweka maeneo yanayofaa kuwa ni maeneo ya kuegesha kwa kupakia na kushusha abiria kwa gari zinazotoa huduma ya usafiri barabarani.