HAPO jana wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla waliadhimisha miaka 49 tangu kuuawa kwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar mzee Abeid Amani Karume hapo Aprili 7 mwaka 1972.

Kufuatia mauaji hayo wananchi wa Zanzibar walikuwa katika dimbwi la simanzi na huzuni katika kiindi hicho cha msiba, ambapo mzee huyo, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiopenda maendeleo ya nchi hii.

Mzee Karume aliuawa wakati jamii ya wazanzibari ikiwa bado ina mahitaji sana kwani katika miaka minane ya uongozi wake alifanya mambo makubwa hadi leo yamebakia kama alamu.

Kabla ya uongozi marehemu mzee Karume, alikuwa ni jabari wa mapinduzi ya Zanzibar baada ya yeye na wenziwe kumng’oa sultani aliyehodhi madaraka.

Kabla ya mapinduzi, maisha baina ya wazawa na jamii ya wageni waliokuwa wakitawala yalikuwa tofauti kwani masultani ndio waliohodhi kila kitu na kuwaacha wazawa bila ya kitu.

Hudima za elimu ya juu ilikuwa chini ya himaya yao, umiliki wa mashamba makubwa ma sekta zote muhimu zilikuwa zikiendeshwa na wao.

Kutokana na hali hiyo Mzee Abeid Karume, akiwa na kundi lake la watu 14 walifanya Mapinduzi na kumuondosha Sultani hapa visiwani.

Akiwa katika uongozi wake wa miaka michache tangu mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1064 ni wazi kuwa ameacha mambo mengi ya maendeleo ambayo hadi sasa yanaonekana kwa macho na kuendelezwa zaidi kwa ustawi wa wazanzibari.

Ahadi  zake ambazo ziliwajaza matumaini wananchi ni sehemu nyengine wa jamii ya wakati huo kuona mwanga wa mabadiliko kwa kuyabadilisha maisha yao.

Kwa hakika, mambo mengi  aliyoyaahidi yalitekelezwa katika kipindi kifupi  kama vile wananchi kuishi katika nyumba za kisasa za Maendeleo kama  za Michenzani, Kilimani, Makunduchi, Bambi na Gamba kwa Unguja na Pemba ni Madungu Chake Chake, Wete na Mkoani.

Hali kadhalika, Mzee Karume aliwajali sana wazee kwa kuwajengea nyumba za kuwatunza zilizoko Sebleni Unguja na Pemba maeneo ya Limbani Wete.

Wazee walithaminiwa na kupewa matunzo stahiki za kimaisha kwani walijengewa nyumba bora huku wakipatiwa huduma kila walizokuwa wanapaswa kuzipata.

Kwa upande mwengine, huduma za afya, elimu na matibabu bure kwa wananchi wote zilipatikana bila bughdha, barabara   za kisasa kwa wakati huo zilijengwa ambapo  mzee Karume alishiriki bega kwa bega na wananchi.

Vile vile jambo kubwa ambalo, mzee Karume alilifanya ni kujenga upendo baina ya jamii na kujenga misingi ya kusaidiana. Ni wazi hadi sasa maendeleo na mambo makubwa aliyoyafanya yanaonekana hadi na kizazi cha sasa.

Mzee Karume ameondoka lakini wakati anazikwa tuliambiwa kilichoondoka ni kiwiliwili chake na mawazo na fikra zake zitadumu milele, hata hivyo kauli hii kiukweli haijatekelezwa kiufanisi.

Pengine baada ya kuondoka mzee Karume Zanzibar ilikumbwa na changamoto kadhaa za kiuchumi kiasi cha ujenzi wa miradi mikubwa kushindwa kuendelea, lakini bado tulipaswa kuainisha mambo ambayo yalipaswa kutekelezwa baada ya Karume.

Maisha ya kiungozi ya mzee Karume ni darasa tosha, lakini viongozi wa kizazi cha sasa mnajifunza mbona mzee huyu hakuwa mbadhirifu lakini saivi tuna baadhi ya viongozi wanahusishwana ufisadi.

Tunachoweza kusema mzee Karume bado hajaenziwa inavyostahiki, hata hivyo tumuombee kwa  Mwenyezi Mungu (S.W) ailaze roho ya marehemu Mzee Abeid Karume mahala pema Peponi Amin.