NA MOHAMED HAKIM

TIMU ya soka ya Kundemba FC inayoshiriki ligi daraja la pili mkoa imefunga mazoezi baada ya hatua ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) kusimamisha baadhi ya mashindano.

Akizungumza na gazeti hili Katibu wa timu hiyo Masoud Maulid Ali alisema kutokana na taarifa walizopewa na ZFF kusimamishwa ligi daraja la pili mkoa na mashindano ya kombe la shirikisho FA wameona hakuna haja ya kuendelea kufanya mazoezi.

“Kiukweli tulijianda kucheza na Mlandege kwa hali yoyote ile na kuendelea kufanya vizuri katika ligi yetu, lakini kutokana na taarifa tuliopewa na ZFF tumelazimika kusimamisha mazoezi mpaka tutakapopata taarifa rasmi kutoka ZFF tutajua tarehe ya kurejea kiwanjani” alisema katibu

Kwa mujibu wa ratiba ya awali Kundemba walikuwa washuke dimbani jana Aprili 8 kucheza na Mlandege kombe la FA na baada ya hapo warudi katika ligi yao ya mkoa na kucheza na New Villa.