MAUAJI, uporaji wa sanaa, wizi wa mafuvu yote ni sehemu ya sauti zinazopazwa kuitaka Ujerumani kutambuwa historia yake ya kikoloni miaka minne baada ya serikali kuahidi kuliangalia upya suala hilo.

“Alama za ukoloni wa kijerumani zipo wazi kabisa kwa mwenye kutaka kuziona”, anasema Naita Hishoono kutoka nchini Nambia.

Ukitembea kwenye mitaa ya mji mkuu wa Namibia, Windhoek, unakutana na majina ya mitaa ya kijerumani, maduka ya kijerumani na hata kanisa lililojengwa wakati wa ukoloni wa mjerumani.

Juu ya yote, unakutana na picha ya kuogofya ya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa jamii za Herero an Nama yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Ujerumani wakati wa ukoloni.

Kwa kila hali, ni ukurasa mbaya sana kwenye kitabu cha historia ambacho kila Mnamibia anakijuwa, lakini ni mada ambayo haipewi uzito wowote nchini Ujerumani.

Kwa Hishoono anayeongoza taasisi isiyo ya kiserikali, National Institute for Democracy, tafauti juu ya namna Wajerumani na Wanamibia wanavyouchukulia uhalifu wa Ujerumani wakati wa ukoloni ni kubwa sana.

“Wanamibia tunaufahamu sana ukoloni kwa sababu tunauona kwenye majengo, tunauona kwenye athari za kiuchumi, tunauona na tunaishi nao kila siku”, alisema Hishoono.

Alieleza kuwa tofauti na wanamibia, wajerumani wamesahau kabisa kwamba nchi hiyo kama iliwahi kuwa na makoloni wa Nambia na ambapo utawala ulisababisha madhara makubwa.

Hata hivyo, mtazamo huo unaungwa mkono na waziri wa Sera ya Utamaduni wa Kitaifa wa Ujerumani, Michelle Müntefering, ambaye alipozungumza bungeni nchini Ujerumani hivi karibuni alisema umewadia wakati wa kuukiri ukweli.

“Sisi, hapa Ujerumani, tumejiachia na dhana kwamba tumetoka kwenye zama za ukoloni tukiwa na vyuma vichache vichakavu ama kwamba ukoloni wa Kijerumani ulikuwa wa muda mfupi mno kuweza kuleta madhara ya muda mrefu”, alisema waziri Müntefering.

Ujerumani ilikuwa taifa la kikoloni kwa muda mchache, ikizikalia nchi za Kiafrika mwishoni mwa miaka ya 1800 na kisha ikapoteza makoloni yake wakati wa vita vya kwanza vya dunia.

Lakini hata ndani ya Ujerumani kwenyewe, bado nyayo za ukoloni huo zingalipo, japokuwa hazijioneshi waziwazi.

Kuna mitaa na masanamu na majengo kadhaa yenye majina ya kuwatukuta Wajerumani wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa zama za ukoloni.

Makoloni ya zamani yanaorodhesha madai ya kazi za sanaa zilizomo sasa kwenye makumbusho za Ujerumani ambazo ziliporwa kutoka mataifa ya Kiafrika wakati wa ukoloni.

Iliichukuwa serikali ya Ujerumani zaidi ya miaka 100 kukiri rasmi matendo maovu ya ukoloni wa nchi hii barani Afrika.

Mnamo mwaka 2018, muungano wa vyama vinavyotawala vya CDU/CSU na SPD ulikubaliana kuchukuwa mtazamo mpya kuelekea historia ya ukoloni ya Ujerumani.

Kwa mujibu wa Müntefering, serikali imechukuwa hatua ya kutunga baadhi ya sheria. Kwa hakika, imeanza hata kuchukuwa hatua mpya, kwa makumbusho za Ujerumani kutakiwa zieleze vipi zinataka kuendelea kushughulikia mali zilizoporwa wakati wa ukoloni.

Kimsingi kabisa, kumeanzishwa kitengo maalum ambacho kinayawezesha makoloni ya zamani kudai kurejeshewa mali zao hizo.

 

Kwa upande mwengine, wanasiasa nao wanazidi kujihusisha na suala hili. Kwa mfano, Waziri wa Utamaduni Monika Grütters amewaalika wadau kwenye mkutano wa kujadiliana hatima ya kazi za sanaa kutoka Benin, ambazo zinachukuliwa kama ngawira ya ukoloni, lakini Nigeria inataka zirejeshwe kwao.

Majumba ya makumbusho yamerejesha mabaki ya mifupa ya binaadamu yaliyoletwa nchini Ujerumani wakati wa ukoloni kwa kile kiitwacho uchunguzi wa kisanyansi.

Miji imeanza kuibadilisha mitaa majina iliyopewa kuwatukuza wakoloni ambapo hivi karibuni ilikuwa ni zamu ya Mtaa wa Wissmann mjini Berlin, ambao ulikuwa umepewa jina la Herman von Wissman.

Kiongozi huyo inasemekana alikuwa mmoja kati ya makatili wakati wa ukoloni dhidi ya waafrika waliotishia kuasi amri za kikoloni kwa kile kilichoitwa Dola la Ujerumani la Afrika Mashariki, mwanzoni mwa miaka ya 1900.

Rais wa Namibia Hage Geingob aliwahi kueleza kuwa nchi yake ipo tayari kupokea msamaha kwa Ujerumani kutokana na mauaji ya halaiki ya enzi za ukoloni dhidi ya watu wa jamii za Herero na Nama.

Rais Geingob alidokeza kuwa Ujerumani inakaribia kuomba msamaha kwa mauaji ya maelfu ya watu wakati wa enzi ya ukoloni.

“Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani imekubali kuwa matukio ya kati mwaka wa 1904 – 1908 yanaweza kutambulika kama mauaji ya halaiki na wako tayari kuomba msamaha, katika kiwango cha juu kabisa cha serikali.” Geingob aliwaambia wabunge.