Ni Mdau mkubwa elimu
Mchango wake ni wa kupigiwa mfano
Aitaka serikali kuwathamini walimu
NA LAYLAT KHALFAN
UNAPOKUTANA nae njiani akili haikutumi kuwa ni msomi aliyebobea na aliyepitia nyadhifa mbalimbali na kubwa serikalini.
Unaweza kusema yule ni mtu tu aliyepindwa na maisha katika miaka yake ya ujana na sasa anasubiri rehema na msaada kutoka kwa wanawe.
Na ukimuona kwenye baraza za kahawa anapasha tumbo moto, utasema yule mzee labda ndo mpishi wa kahawa kutokana na ucheshi wake na ukarimu uliotukuka.
Nimesema hivyo kutokana na mazingira yake niliyomkuta kijijini kwao Ndaambani, shehia ya Dimani, wilaya ya Magharibi, Unguja.
Waasifu wake ana umbo la wastani, mrefu kiasi na tayari ameshakuwa mtu mzima anaejiweza, aliyeng,oa baadhi ya meno yake mbele na kwa haraka haraka utasema ni mzee aliyekuwa hajasoma.
Kumbe umdhaniae siye kumbe ndiye, ni gwiji wa sayansi hapa Zanzibar na mchango wake ni mkubwa sana katika fani hiyo.
Uvaaji wake wa kanzu, seruni na kofia utasema ni mtu aliyekuwa anacheza ngoma ya kibati, kumbe huvaa tu wakati anapokuwa katika mazingira ya kwao.
Nimekutana nae kwa mara ya kwanza , lakini nimemjua kuwa ni mtu anaependa mas-hara kwa watu na anazungumza na kila rika bila ya kujali usomi na elimu aliyokuwa nayo.
Huyo ni Maalim Ameir Suleiman Haji (Njeketu), ambaye ni mwalimu maarufu sana na aliyefanikiwa kuwasomesha wananfunzi wengi wa Sayansi hapa Zanzibar hasa masomo ya Kemia na Fizikia (Chemistry na Physics).
Uwezo wake mkubwa wa masomo hayo amesaidia wanafunzi wengi wa Zanzibar na kupasisha katika ngazi mbali mbali za elimu.
Akizungumza na makala haya Maalim Njeketu anasema kuwa safari yake kuwa mwalimu wa Sayansi ni ndefu na hakutarajia kuwa hivyo, lakini alilenga zaidi kuwa Mhandisi.
Anasema baada ya kumaliza masomo yake ya Kidatu cha Sita mwaka 1974, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya Sayansi kwa kuwa tayari alikuwa amejikita zaidi katika masomo ya Kemia na Fizikia.
Aidha anasema kuwa moyoni mwake alikuwa awe Mhandisi, lakini alishajiishwa awe hivyo kuwaq bingwa wa masomo hayo.
Anaeleza kuwa alipomaliza masomo yake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikusita haraka ilimuajiri na kumpeleka Chuo cha Ualimu Nkrumah wakati huo mwaka 1978 na kusomesha waliokwenda kwa kozi za Ualimu na pia Kidatu cha Nne kwa wakati huo.
Hata hivyo, anasema mnamo mwaka 1986 alipata uhamisho na kwenda Skuli ya Sekondari ya Benbella kama Mwalimu Mkuu kwa muda wa mwaka mmoja tu, na kupata uhamisho kwenda Sekondari ya Lumumba kuendelea kusomesha somo la Fizikia na Kemia.
Anasema kwa kuwa alikuwa mbobezi wa masomo hayo, alisomesha vizuri na kuipatia sifa skuli ya Lumumba kwa kufanya vyema kitaifa mara kadhaa na hadi leo skuli hiyo bado inaendelea kupasisha vizuri siku hadi siku.
“Inawezekana baada ya kufanya vizuri skulini hapo nilibahatika kuchaguliwa kuwa Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo”, alisema Maalim Njeketu akionesha kujivunia heshima hiyo aliyoipata kwa mafanikio.
Anasema kwa vile kazi ya ualimu ni ya kuhama hama haikuchuka muda mrefu alihamishiwa tena Chuo cha Ualimu Nkrumah na alidumu kwa muda wa miaka mine.
Aidha anasema akiwa katika chuo hicho ndipo alipojizolea umaarufu zaidi , kwani alipangiwa kazi na kuwa Mkuu wa Divisheni ya Sayansi na Teknolojia.
Anasimulia kuwa kadri siku zilivyokwenda alikuwa ni mwalimu wa kupigiwa mfano kioo kutokana na jitihada zake za ufundishaji na kwa bahati Rais aliyekuwepo madarakani wakati huo alimpandisha daraja na kuwa Mkurugenzi wa Elimu Zanzibar.
Anaeleza kuwa mnamo 2006 akateuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Kabla ya kustaafu nafasi yake ya mwisho alikuwa Mkurugenzi wa Baraza la Mitihani ya Zanzibar.
Baada ya kufanyakazi zake vizuri katika miaka yote hiyo,Maalim Njeketu anasema kuwa hakutarajia kupata heshima kubwa ya nchi , lakini kumbe jitihada zake zilikuwa zinaonekana.
Anasema Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa Awamu ya Saba, Dk. Ali Mohamed Shein alimtunuku nishati ya utumishi ulitukuka katika sherehe maalum wakati wa sherehe za Mapinduzi.
“ Sikutarajia shangwe, nderemo na vigeregere vilisikika baada ya wakati wa kukabidhiwa nishani hiyo kuonesha kuwa kweli jitihhada zangu zilithaminiwa”, alifahamisha Maalim Njeketu huku akionesha kweli alithaminiwa mchango wake.
Mwalimu Njeketu ameiambia makala haya kuwa licha ya jitihada na uzoefu mkubwa aliokuwa nao katika fani ya Ualimu, lakini alivunja ukimya na kusema hazikuwa ndoto zake za kusomesha katika maisha yake, lakini serikali ndio iliyomtaka kujikita na fani hiyo na aliitikia.
“Zamani kazi zilikuwa zinatafuta watu na sio leo watu wanatafuta kazi. Kwa hiyo baada ya kumaliza chuo tu nilipendekezwa niwe mwalimu na sikuweza kupinga na nilifanya hivyo”, aliongeza.
Anasema ndoto zake alikuwa anataka awe injinia na ndio maana alijikita zaidi katika masomo ya sayansi.
“Nilipangiwa kazi hii ya kusomesha na sikua na kipaji nacho na nililazimika kusomesha kwa kuwa serikali iliamua mimi kufanya hivyo”, anasema.
Maalim Njeketu anasema katika fani yake hiyo ya ufundishaji alibahatika kutembelea nchi mbali mbali kama vile China, Marekani, Ufaransa, Afrika Kusini, Zimbambwe, Uganda, Israel, Pakistan na kadhalika kwa lengo la kupata uzoefu wa kusoma na kusomesha pia.
Anasema katika nchi hizo alizotembelea alibahatika kuwasomesha wanafunzi wengi, ambao wengi wapo kwenye serikali katika nafasi kubwa.
Anasema kwa hapa Zanzibar amesomesha wengi ambao wameshika nyadhifa mabali mbali zikiwemo za Ukurugenzi, Ukatibu Mkuu makamanda wa jeshi, walimu na hata madaktari wakubwa.
Akiwataja baadhi ya wanafunzi wake aliopasisha kuwa wakubwa ni Maryam Abdallah Sadala (Mabodi), ambae ameshika nafasi ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Dk.Ota ambae ni daktari bingwa wa watoto.
Wengine ni Hassan Aboud Talib alikuwa TRA, Asya Iddi ambae kwa sasa ni Mkurugenzi wa Elimu Sekondari na wengine ambao hakuweza kuwamaliza kuwataja.
Aidha Maalim Njeketu hakusita na kuiomba serikali kuendelea kuwathamani wastaafu hususan walimu kwa kuwatizama kwa jicho la huruma na kuwaweka katika nafasi yao.
“ Walimu katika nchi ndio kila kitu. Ndio msingi wa fani zote zinazohitajika”, alisisitiza.
Vile vile aliiomba serikali kujitahidi kushughulikia zaidi suala la elimu kwa kuwapatia nyezo walimu na wanafunzi kwa kuwaimarishia maabara za sayansi na lugha, upatikanaji wa vitabu na vitendea kazi vya walimu.
Kwa upande mwengine alisisitiza kwamba masomo ya Sayansi na somo la Hisabati kusomeshwa walimu wengi ili maendeleo ya elimu yaweze kufikiwa.
Maalim Njeketu alizaliwa mwaka 1953 katika kijiji cha Dimani, wilaya ya Magharibi Unguja.
Mnamo mwaka 1961 alijiunga na Skuli ya Msingi Kombeni kuanzia darasa la kwanza hadi Kidato cha Pili.
Mwaka 1971 alibahatika kuingia Skuli ya Sekondari Lumumba kuanzia Kidato cha Tatu hadi cha Sita na kumaliza masomo yake hapo 1974.
Maalim Njeketu ana watoto watano wakiume wanaume watatu na wawili wanawake, huku mwanae mmoja wa kiume akiwa amefuata nyayo zake za Ualimu na anasomesha katika skuli ya Lumumba masomo ya Sayansi.
“Nimestaafu kazi mwaka 2016 hadi leo ndio nipo hapa naishia kwenye vijiwe vya kahawa na kupoteza muda huku serikali ikiwa ndio mama anaeniendeleza kunilea”,anasema.
“Nashkuru wanangu wote wamenifuata mimi nathubutu kusema wamenipita kielimu, kwani wao wamefikia hadi PhD”, anamalizia Maalim Njeketu, ambaye ni hazina kubwa ya Taaluma ya Ualimu.