NAIROBI, KENYA

MASKOFU wa kanisa katoliki nchini Kenya, wameiomba serikali ya nchi hiyo kuacha msimamo wake wa kutaka kuzifunga kambi za wakimbizi wa kisomali zilizomo nchini humo.

Hivi karibuni serikali ya Kenya iliibuka na msimamo na kutoa siku 14 kambi za wakimbizi wa Dadaab na Kakuma zenye jumla ya wakimbizi wapato 410,000 ziwe zimeshafungwa.

“Ni bahati mbaya sana kusikia serikali kwa muda mfupi sana inataka kuzifunga kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma, hawa watu wanataka huduma nadhani serikali ingeregeza msimamo”, alieleza askofu Philip Anyolo wakati akitoa taarifa ya baraza la maaskofu.

Hivi karibuni mahakama kuu nchini Kenya ilisitisha hatua ya serikali nchi hiyo kufunga kambi mbili za wakimbizi.

Jaji Antony Mirima alitoa agizo la muda baada ya aliyekuwa mgombea urais Peter Gichira kuwasilisha changamoto ya kisheria kutaka kuzuia kufungwa kwa kambi mbili za wakimbizi.

Wizara ya mambo ya ndani Kenya ilikuwa imewapa idara ya kuhudumia wakimbizi ya Umoja wa Mataifa-UNHCR kuagiza kubuni mpango wa kufunga kambi hizo.